BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
BILIONEA Mohamed Dewji 'Mo' amezidi kufanya mambo kimya kimya ndani ya klabu ya Simba na sasa amewaahidi kuwasaidia kulipa Sh 80 milioni ili waweze kutoa nyasi zao zilizozuiwa bandarini, pesa hiyo ni kwa ajili ya malipo ya kodi ya nyasi hizo zilizotoka China.

Uongozi wa Simba umeshindwa kupata fedha hizo na kutoa nyasi ingawa walijaribu kufanya jitihada za kuandika barua serikalini ya kuomba punguzo la kodi hiyo lakini wamegonga mwamba kwani serikali ya Rais John Magufuli ipo makini kwenye suala zima la ulipaji kodi.

Simba tayari wameanza ujenzi wa uwanja wao uliopo Bunju na kinachosubiriwa ni kuwekwa nyasi hizo ambapo tayari fundi atakayetandika mkeka huo amepatikana kutoka China hivyo nyasi zitakapotolewa tu naye atatua nchini.Mipango ya viongozi wa Simba ni kuanza kuutumia uwanja huo kwa ajili ya mazoezi kati ya Desemba au Januari huku taratibu nyingine zikiendelea ambazo zimepangwa kuwepo kwenye eneo lao hilo lenye hekari 19.

Alipoulizwa Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu alisema kuwa; "Kuna taratibu zinafanywa kwa ajili ya kutoa nyasi zetu bandarini japokuwa Mo ametuahidi kutusaidia, nadhani hili litatatuliwa mapema tu."


Post a Comment

 
Top