BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
UONGOZI wa klabu ya Mwadui FC umepanga kumtangaza Kocha wao mpya Jumapili ijayo ili achukue mikoba iliyoachwa na  Jamhuri Kihwelo 'Julio' aliyejiuzulu wiki iliyopita kutokana na kutoridhishwa na maamuzi ya marefarii.

Uongozi huo umesema kuwa tayari umepokea barua rasmi toka kwa Julio ya kutaka kujiuzulu na wamekubali ombi hilo huku mchakato wa kumpata mrithi wake ukiendelea na Jumapili ijayo watamtangaza atayechukua mikoba yake.

Katibu mkuu wa klabu hiyo Ramadhani Kilao ameiambia BOIPLUS kuwa wamepokea maombi mengi kutoka kwa makocha mbali mbali ya kutaka kukinoa kikosi chao na uongozi unapitia majina hayo kwa  umakini mkubwa kabla ya kumtangaza siku hiyo ya Jumapili.

"Julio katuletea barua rasmi ya kujiuzulu na pia tumepokea maombi mbali mbali kutoka kwa makocha ambao wanataka kuja kufundisha, mchakato unaendelea na tutawatangazia muda si mrefu," alisema Kilao.

Kilao alisema wanafanya haraka kupata mrithi wa kocha huyo ili kusiharibu mlolongo mzima wa 'Wachimba madini' hao kutokana na ligi kuwa mbichi kwakua ndiyo wameshuka dimbani mara saba pekee.

"Mchakato tunataka uende haraka ili timu isiyumbe kwakua hatukuwahi kufikiria kuwa Kocha wetu atatuacha katika kipindi hiki," alisema Kilao.

Post a Comment

 
Top