BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
LICHA ya kocha wa Mwadui Jamhuri Kihwelo 'Julio' kutangaza kujiuzulu kufundisha soka kutokana na maamuzi mabovu ya marefa, Uongozi wa klabu hiyo umesema hauna taarifa rasmi na bado wanamtambua kama mwalimu wao.

Julio alitangaza maamuzi hayo jana baada ya kushuhudia vijana wake wakipokea kichapo cha bao 1-0 toka kwa Mbeya City mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo alikiri kuwa marefa wamekuwa wakichezesha huku wakiwa na matokeo tayari na licha ya yeye kukemea mara kwa mara lakini imeshindikana.

Katibu Mkuu wa Mwadui Ramadhani Kilao ameiambia BOIPLUS kuwa Julio hajawaandikia barua ya kujiuzulu wala hakupeleka taarifa yoyote rasmi ya kujiengua huko hali inayoonyesha kuwa bado anaendelea na majukumu yake.

"Hakuna taarifa yoyote rasmi aliyotuletea hadi sasa, tumesikia kwenye vyombo vya Habari kuwa amejiuzulu lakini hakutuandikia barua kwahiyo bado tunamtambua kama kocha wetu," alisema Kilao.

Katibu huyo aliongeza kuwa endapo Kocha huyo atawapelekea barua ya kujiuzulu hawatamzuia kufanya hivyo kwakua ndiyo maamuzi aliyofikia na watampa mkono wa kwaheri.

"Akileta barua ya kutaka kuondoka sisi hatutakuwa na njia za kumzuia na tutayaheshimu maamuzi yake," alimaliza Kilao.

Post a Comment

 
Top