BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
STRAIKA wa Simba, Laudit Mavugo ameanza kupunguza makali yake ya ufungaji mabao tofauti na alipokuwa kwao Burundi akiwa Mfungaji Bora kwa miaka miwili mfululizo jambo lililowashawishi viongozi wa Simba kufunga safari na kumpa mkataba ila mdogo wake Cedrick Mavugo amesema kaka yake anapaswa kurudi kwao kwanza ndipo kiwango chake kitapanda na kuifungia Simba mabao mengi tu.Mavugo amekuwa akishindwa kufunga hata kama yupo katika nafasi nzuri huku wengine wakieleza kuwa wakipangwa pamoja na Ibrahim Ajib kila mtu anakuwa mchoyo kutoa pasi kwa mwenzake mwenye nafasi nzuri ya kufunga matokeo yake husababisha timu kushindwa kupata  mabao ya haraka tofauti na pale ambapo mmoja huanzia benchi.

Akizungumza na BOIPLUS Mavugo Jr alisema kuwa anaamini kaka yake atafunga tu hasa akirudi kwao ingawa hakutaka kufafanua zaidi kuwa arudi kuchukuwa ujuzi gani ila yeye alisisitiza kuwa Mavugo anapaswa kurudi kwanza kwao ndipo aje acheze Simba.
Cedric Mavugo, ndugu wa mshambuliaji wa Simba, Laudit Mavugo
"Nakwambia atafunga tu ngoja arudi huku nyumbani, tena atafunga mabao mengi sielewi kitu gani kimempata sasa hivi mpaka ashindwe kufunga mechi zote alizocheza, akija utaona tu maana mambo mazuri hayahitaji haraka," alisema Mavugo Jr ambaye anaichezea timu ya Black Eagle 'Aigle Noir' inayoshiriki Ligi Kuu ya Burundi.

Wakati Mavugo Jr akiwapa matumaini mashabiki wa Simba kuwa Mavugo atafunga sana, straika wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel naye alisema kuwa; "Namkubali sana kiwango chake ila kuna mambo mawili kwake anayotakiwa kuyafanyia kazi haraka, kuacha uchoyo na kupambana halafu asifikirie kwamba ushindani ni uwanjani tu hata nje ya uwanja.

"Mavugo ni straika mzuri na ninamwelewa sana ila anaamini uwezo wake mkubwa wa kucheza huku akisahau kupambana kwa kila hali, bado ana nafasi na asikate tamaa anapaswa kufanya marekebisho ya haraka," alisema Gabriel.

Post a Comment

 
Top