BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
SIKU moja baada ya Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans Pluijm kujiuzulu kufundisha mabingwa hao wa ligi kuu na Kombe la FA, Msaidizi wake Juma Mwambusi nae ameamua kufuata nyayo zake kwa kujiweka pembeni na sasa anatajwa kujiunga na Prisons.

Taarifa za kujiuzulu kwa Pluijm ziliripotiwa kwa mara ya kwanza na mtandao huu wa BOIPLUS jana ikiwa ni masaa machache baada ya Kocha Mzambia George Lwandimina kuwasili nchini huku ikisemekana tayari amesaini mkataba wa miaka miwili na Mabingwa hao pasipo kumpa taarifa yoyote Pluijm jambo ambalo limeonekana kumkera.

Mitandao mbalimbali ya kijamii na vyombo vya habari jana pia vilitoa taarifa juu ya kujiuzulu kwa wataalamu wote wa benchi la ufundi akiwemo Mwambusi ambaye anadaiwa sasa kusubiri tu mafao yake ili aende kujiunga na Prisons inayofundishwa na Meja Mstaafu Abdul Mingange ambaye mkataba wake unamalizika Desemba kwani alisaini mkataba wa miezi sita tu.

Mwambusi aliwahi kuifundisha timu Mbeya City kwa mafanikio makubwa ambapo aliisaidia kumaliza timu hiyo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa ndiyo imepanda daraja msimu 2013/14 na kuwafanya City kuwa tishio hata kwa timu kubwa za Simba na Yanga.

"Mwambusi naye amebwaga manyanga anasubiri apewe chake aende zake Prisons kutokana na kutoridhishwa na maamuzi yaliyofanywa na uongozi wa klabu hiyo ya kumleta kocha mpya huku wao wakipata taarifa kutoka kwenye vyombo vya Habari," kilisema chanzo chetu.

Mapema asubuhi ya leo Kaimu Katibu mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alinukuliwa na Radio moja akisema baada ya Kocha Hans kujiuzulu mikoba itachukuliwa na Mwambusi hadi atakapopatikana Kocha mpya huku wakiendelea kufanya siri kubwa kuhusu kusaini mkataba na Mzambia Lwandimina.

Mwambusi mwenyewe alisema bado hajapata taarifa rasmi kutoka kwa uongozi juu ya kukaimu nafasi ya Kocha mkuu huku akisema kesho anatarajia kwenda klabuni kuonana na Uongozi na ndiyo itajulikana kama ataendelea na mabingwa hao au atajiweka pembeni.

Zaidi ya wiki moja na nusu kumekuwa na taarifa za mabingwa hao kutaka kubadili benchi zima la ufundi lakini Uongozi wa Yanga umekuwa ukikanusha madai hayo na kuwataka Wanachama wao kupuuza tetesi hizo lakini kwa zaidi ya asilimia 90 zinaelekea kukamilika.

BOIPLUS inafahamu kuwa Lwandamina raia Zambia atakuwa Kocha mkuu akisaidiwa na Charles Mkwasa, Peter Manyika akiwa kocha wa makipa huku Sekilojo Chambua akiteuliwa kuwa Meneja wa timu. Imeelezwa kuwa Lwandamina atarejea kwao kwa ajili ya kumalizana na Zesco kwani mkataba wake haujamilizika na ndipo atakaporudi kujiunga na Yanga.

Post a Comment

 
Top