BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
MSHAMBULIAJI wa Toto African, Waziri Junior amesema kwamba ukuta wa Simba ulioongozwa na Method Mwanjali, Juuko Murshid ndiyo ulimharibia mahesabu na kujikuta akiishia kutengeneza nafasi tu kwa wenzake labda wangeweza kutikisa nyavu za wapinzani wao katika mechi yao iliyochezwa wiki iliyopita ambapo walilala bao 3-0.

Mbali na mabeki hao wazoefu pia ukuta wa Simba uliongezewa nguvu mara mbili na Mohamed Hussein 'zimbwe Jr' anayecheza kushoto pamoja na Janvier Bokungu anayekuwa upande wa kulia waliweza kumdhibiti mfungaji bora huyo wa Toto msimu uliopita.

Waziri aliyetokea timu ya vijana ya Simba, alisema kuwa mambo yalikuwa magumu kwake kuweza kupenya ngome ya Simba ndipo alipoamua kubadilisha mawazo ya kufunga na kuanza kutengeneza nafasi ingawa wenzake hawakuwa makini katika umaliziaji.

"Mabeki wa Simba walikuwa makini sana maana walikuwa hawanipi nafasi, hivyo badala ya kufunga nikawa natengeneza nafasi kwa wenzangu ili wafunge ila walikosa umakini, mabeki walikuwa wanakuja kwangu wawili ama watatu kila ninapogusa mpira maana walijua ningeweza kuleta madhara langoni mwao," alisema Waziri.

Toto imepoteza mechi hiyo na sasa inakwenda kuzikaribisha timu mbili kwenye uwanja wa CCM Kirumba, wageni wao ni Azam FC na Mtibwa Sugar ila mchezaji huyo amesema watapambana kuhakikisha pointi sita zinabaki kwao maana hali yao ni tete kwani wana pointi nane pekee walizokusanya kwenye mechi 12 walizocheza.

"Matokeo yetu ni mabaya sana na yanakatisha tamaa, ila hatutaki kuikubali hali ya kukata tamaa kwasasa hivyo tutapambana mpaka mwisho, naamini mimi na wenzangu bado tuna nafasi ya kuisadia timu isishuke daraja ila tunaomba ushirikiano mkubwa wa mashabiki na viongozi wetu wawe na umoja, tumebakiwa na mechi tatu mzunguko huu kwa ushirikiano wa pamoja tunaweza kushinda zote," alisema Waziri.

Post a Comment

 
Top