BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar
WAKATI beki Method Mwanjali anasajiliwa miezi michache iliyopita, mashabiki wengi wa soka na hasa wale wa Simba walipata hofu juu ya uwezo wake huku wengi wakizungumzia kuhusu umri wakidai kuwa umekwenda sana hivyo hatoweza kupambana na washambuliaji chipukizi na wale wazoefu.

Hali imekuwa tofauti ambapo sasa Mzimbabwe huyo amegeuka kuwa roho ya safu ya ulinzi ya Wekundu hao huku akiwa amecheza mechi zote za Ligi Kuu tangu ianze tena bila kufanya makosa ya kizembe yaliyoigharimu timu.

Kocha wa timu hiyo Joseph Omog raia wa Cameroon, amekuwa akimtumia yeye kama kisiki huku Novaty Lufunga na Juuko Murshid wakipokezana katika kumpa msaada mkongwe huyo asiye na papara wala mambo mengi uwanjani.

Mashabiki wa timu hiyo sasa wanaamini kuwa ukuta wao umepata 'Afsa Usalama' wa uhakika na ndio sababu umeruhusu mabao matatu tu huku timu hiyo ikiwa haijapoteza mchezo wowote katika mechi saba za ligi ilizocheza.
Mweka hazina wa kundi la Simba Spora, Mbwana Masaninga kushoto akimkabidha pesa Sh. 400,000 Method Mwanjali

Katika kuthibitisha furaha na imani yao kwa Mwanjali, kikundi cha mashabiki na wanachama wa Simba kutoka matawi mbalimbali maarufu kama Simba Spora, jana kimemtangaza kuwa mchezaji bora wa mwezi Septemba huku wakimpatia Sh 400,000 kama zawadi.

Kundi hilo ambalo asili yake ni katika mtandao wa kijamii wa Whatsapp limekuwa likichagua mchezaji bora wa kila mechi na mwisho kumtangaza mchezaji bora wa mwezi ambaye huzawadiwa pesa taslimu.

Post a Comment

 
Top