BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KIUNGO Mzamiru Yassin ameonyesha sababu ya viongozi wa Simba kumsajili kutoka Mtibwa Sugar baada ya kutandaza soka safi na kusaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Toto African huku yeye mwenyewe akifunga mawili.

Tangu asajiliwe Mzamiru amecheza mechi zote 11 na kujihakisha namba kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Joseph Omog na mpaka sasa tayari ameifungia Simba mabao manne likiwemo lile la ushindi dhidi ya Mbao FC katikati ya Juma lililopita.

Toto waliingia uwanjani wakiwa na lengo la kuzuia huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza kitu ambacho walikimudu katika dakika 40 za mwanzo huku ikionekana Kocha wao Mjerumani Tim Jost aliwataka vijana wake kutoruhusu bao la mapema ili wasicheze kwa presha.

Mzamiru aliwapatia Simba bao la kwanza dakika ya 42 baada ya kupokea pasi toka kwa Fredrick Blagnon ambaye alifanya kazi kubwa ya kuwahadaa mabeki wa Toto kabla ya kumpasia mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa ambaye bila ajizi aliutumbukiza kimiani na kumuacha golikipa Mussa Kirungi akiwa hana lakufanya.Laudit Mavugo alitumia dakika tano kuipatia Simba bao la pili tangu kuingia uwanjani kuchukua nafasi ya Blagnon aliyeumia kichwani baada ya kugongana na mchezaji mmoja wa Toto katika harakati za kuzuia mpira alipomalizia kazi nzuri ya Mohamed Ibrahim.

Mzamiru tena aliifungia Simba bao la tatu baada ya kumalizia mpira wa kona uliopigwa na beki Janvier Bokungu ulioguswa kidogo na Ibrahim na kumkuta mfungaji huyo akiwa peke yake.

Simba wameendelea kujikita kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha alama 29 baada ya kushuka dimbani mara 11.

Post a Comment

 
Top