BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
WAZIRI wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la uchangiaji wa damu linaloratibiwa na Tegemeo Arts Group Tanzania litakalofanyika Disemba 25 kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Tamasha hilo litawapambanisha Wasanii nguli wa muziki wa Taarab Bi Mwanahawa Ally, Hadija Kopa pamoja na Hadija Yusuph ili kujua nani atazikonga nyoyo za mashabiki wa mahadhi ya Pwani watakaohudhuria katika tamasha hilo.

Mratibu wa Tamasha hilo Hamis Abdallah 'Kajumulo' amewaambia waandishi wa Habari kuwa mbali na uchangiaji huo wa damu pia kutakuwa na zoezi la upimaji wa afya kwa hiyari kwa watakojitokeza huku sehemu ya mapato ikitumika kuchangia wanafunzi 100 kutoka mikoa mbali mbali nchini vifaa vya elimu kama sare, vitabu na viatu.

"Sehemu ya mapato tutachangia wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu hasa vijijini ili kuinua sekta ya elimu nchini kwa ajili ya kusaidia jitihada za Rais wetu John Magufuli," alisema Kajumulo.


Kwa upande wake Kopa ambaye ni miongoni mwa washindani kwenye tamasha hilo alisema amevutika kushiriki tamasha hilo ili kuwasaidia wenye matatizo ya damu hasa Wanawake huku akiwataka wanaoshindana naye wakae vizuri kwavile amejipanga kuwapoteza vibaya uwanjani hapo.

"Nitawaonyesha kwa kwanini mimi naitwa Malkia wa Mipasho nchini, nitawafunika vibaya Bi Mwanahawa na mdogo wangu Hadija lazima niwaambie ukweli ili wajiandae," alitamba Kopa.

Wasanii hao watasindikizwa na Msondo Ngoma, Sikinde, Jahazi Modern Taarab, Ogopa Kopa Classic Band, The East African Melody pamoja na Five Stars Modern Taarab.

Wengine ni Afande Sele, 20%, Samir, Wali Nazi, Wakali wa Mchiriku TAGT Music, Wakali wa Singeli, Mtanga, Bambo na Kiwewe.

Post a Comment

 
Top