BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
Mwandishi wa BOIPLUS akifanya mahojiano na Nyoshi El Saadat leo

VYOMBO vya Habari nchini vimelaumiwa kushusha thamani ya muziki wa dansi  uliokuwa unapendwa zaidi miaka ya 2000 na watu wa rika zote baada ya kutumia nguvu nyingi zaidi kuupandisha muziki wa kizazi kipya 'Bongo Fleva'.

Rais wa bendi ya FM Academia Nyoshi El Saadat ameiambia BOIPLUS kuwa adui mkubwa wa muziki wa dansi nchini ni vyombo vya Habari kutangaza zaidi Bongo Fleva mpaka kuwakaririsha wadau kuwa hakuna muziki mzuri mwingine zaidi ya huo kitu ambacho hakina ukweli wowote ndani yake.

Nyoshi ambaye ni shabiki mkubwa wa timu ya Simba na Real Madrid ya Hispania alisema muziki wa dansi bado unafanya vizuri na wanafanya maonesho kila wiki maeneo mbali mbali lakini vyombo vya Habari vipo bize na Bongo Fleva.

"Nyinyi watu wa Habari ndiyo mlioshusha Dansi na mkiamua mnaweza kuirudisha kwenye ramani ya muziki nchini lakini mkiendelea na Bongo Fleva yenu basi sisi tutaonekana hakuna tunachofanya," alisema Nyoshi.

Mkongomani huyo alisema FM Academia ni tofauti na bendi zote nchini kama Akudo, Twanga Pepeta, Mashujaa Music, Double M Sound na nyinginezo kutokana na upekee wao katika utunzi, uchezaji hadi kuimba ambapo kila siku wanabadilika kutokana na wakati huku wengine wakibaki vile vile na kuwafanya mashabiki kuwaona hawana jipya hali ambayo ni tofauti sana na wao.

Bendi hiyo inaundwa na nyota kibao kutoka nchini DR Congo wakiwemo Nyoshi mwenyewe, Patcho Mwamba, Pablo Masai, Jesus Katumbiz, Ben Mbiyevanga, Thelathini na tatu, Elombe Kijinja na wengineo ambapo album yao mpya inayoitwa 'Chuki ya nini' ikiwa tayari ipo madukani.

Post a Comment

 
Top