BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
BEKI kisiki Juma Nyosso bado anaendelea kusota mtaani huku akisubiri huruma ya Kamati ya Sheria, haki za wachezaji iliyo chini ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ingawa bado kuna giza kubwa katika suala lake.

Hivi karibuni beki huyo aliyefungiwa miaka miwili kwa kosa la utovu wa nidhamu alipeleka barua katika Shirikisho hilo kuomba msahama akijutia kosa hilo na kwamba asamehewe ili aweze kuendelea na soka lake kwani hiyo ndiyo ajira pekee aliyonayo.

Hata hivyo suala lake bado halijajadiliwa baada ya kamati hiyo kuahirisha kesi mbalimbali zilizokuwa chini yake ambazo bado hazijapangiwa siku.

Meneja wa mchezaji huyo ambaye aliwahi kuichezea Simba, Taifa Stars na Mbeya City, Herry Mzozo aliiambia BOIPLUS kuwa maisha ya Nyosso nje ya soka yanaendelea kuwa magumu kwani TFF ndiyo iliyoshikilia hatima yake.

"Hatuna namna nyingine zaidi ya kusubiri hiyo Kamati ikutane, Nyosso aligundua makosa ndiyo maana aliandika barua ya kuomba msamaha, Nyosso alikuwa anategemea soka kuendesha familia yake yenye watoto wawili ila sasa yupo kwenye wakati mgumu sana.

"Tunaamini Kamati itasikiliza ombi la Nyosso adhabu aliyopewa ni kubwa na sasa anastahili kusamehewa ili arudi uwanjani ingawa haijulikani ni lini litasikilizwa ombi hilo," alisema Mzozo.

Tangu afungiwe, Nyosso sasa ameingia kutumikia mwaka wa pili kwa kosa la kumdhalilisha straika wa Azam, John Bocco huku akishindwa kabisa kulipa Sh 2 milioni alizotakiwa kulipa ikiwa ni faini yake iliyoambatana na adhabu hiyo.

Post a Comment

 
Top