BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
KOCHA wa zamani wa Simba, Mzambia Patrick Phiri anaijua vizuri Ligi Kuu ya Vodacom maana ameifundisha Simba kwa nyakati tofauti na kuipa mataji mara mbili ila amemwambia Mzambia mwenzake George Lwandamina afanya kazi kwa uadilifu kwa kulinda uwezo wake ili afanikiwe ingawa ameipa nafasi zaidi Simba kuwa inaweza kutwaa 
ubingwa kama wataendelea na utulivu huo.

Lwandamina ambaye ni kocha mkuu wa Zesco alitua nchini  hivi karibuni kwa ajili ya mazungumzo na Yanga huku ikidaiwa kuwa tayari amesaini mkataba wa miaka miwili ambapo ataanza kuifundisha Yanga Novemba Mosi na sasa amerudi Zambia kwa ajili ya kumalizana na uongozi wa timu yake. Mholanzi Hans Pluijm aliyeipa Yanga ubingwa mara mbili mfululizo tayari alijiuzulu.

Pluijm ameondoka Yanga akiiacha timu yake ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 24 wakati Lwandamina ambaye jana timu yake ya Zesco ilifungwa na Nkwazi bao 1-0 na yeye akiwa benchi ingawa siku ya mazoezi ya 
mwisho timu hiyo ilikuwa na wasaidizi wake matokeo hayo yamewafanya wawe nafasi ya tano wakiwa na pointi 50.

Zesco itaingia uwanjani keshokutwa Jumamosi kucheza na Green Buffaloes kwenye uwanja wa Jeshi mjini Lusaka na hiyo inaweza kuwa mechi ya mwisho kwa Lwandamina kukaa benchi kwani atatakiwa kuja kuanza kazi Yanga kwani imeelezwa kwamba tayari kocha huyo ameonyesha wazi kutaka kuondoka kwenye timu hiyo.

Habari kutoka ndani ya klabu ya Zesco zinasema kuwa kocha huyo amewakubali kutua Yanga baada ya kukubali kulipwa mshahara mara mbili ya ule anaolipwa Zesco na kwamba hivi sasa mzunguko wa pesa nchini humo umekuwa mgumu kuliko hapa 
nchini na hiyo ndiyo sababu kubwa inayomkimbiza Lwandamina.


Akizungumza na BOIPLUS, Phiri ambaye anaifundisha timu ya Forest Rangers inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia, alisema kuwa Lwandamina ni kocha mzuri ila anapaswa kuendana na mifumo ya soka la Tanzania ikiwemo mfumo wa viongozi wa timu kubwa kama Yanga.

"Yanga na Simba ni timu kubwa, ni timu ambazo zina mambo mengi hivyo ukiwa kocha wa timu hizo unapaswa kuwa na misimamo yako lakini bila kukiuka taratibu zao. Namfahamu Lwandamina ni kocha mzuri na atawasaidia sana Yanga kikubwa ni kumwacha afanye majukumu yake yaliyompeleka pale," alisema Phiri ambaye keshokutwa Jumamosi timu yake inayoshika nafasi ya nane ikiwa na pointi 40 itacheza na Zanaco.

Akizungumzia mwenendo wa timu yake ya zamani, Phiri alisema; "Wakienda hivyo kwa hakika Simba watatwaa ubingwa msimu huu, wapo nafasi nzuri na timu yao si mbaya nimekuwa nikiifuatilia mara kadhaa ingawa sio sana, wasikubali msimu huu upite pasipo kutwaa ubingwa."

Post a Comment

 
Top