BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Mbeya
MBEYA City imeshindwa kutamba kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya kukubali sare tasa na Stand United lakini kocha wa City, Kinnah Phiri ametamba kuwakamata wapinzani kila idara ingawa safu yake ya ushambuliaji bado imeendelea kuwa butu huku akiwatetea kuwa uchanga wao ndiyo unawafanya washindwe kufunga.

Phiri amesema sasa anaelekeza nguvu zake kwenye mechi yao ijayo dhidi ya Simba ambapo watawakaribisha Jumatano ya wiki ijayo kwenye uwanja huo huo wa Sokoine huku Stand wao wanarudi Shinyanga kujiandaa na mechi yao dhidi ya Azam Fc.

Mbali na ubutu wa safu yake, Phiri ameiambia BOIPLUS kuwa timu yake ingeshinda mabao hata manne kipindi cha kwanza huku akimlalamikia mwamuzi wa mechi hiyo kuwanyima bao lao lililofungwa na mshabuliaji wake Omary kwa madai kuwa aliotea.

"Unajuwa washambuliaji wangu wengi ni wachanga hivyo wana matatizo ya kushindwa kumalizia mpira hata wanapokuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga ila nitakwenda nao taratibu hadi watakuwa wafungaji wazuri wanapiga mipira mizuri lakini inaishia kugonga mwamba.

"Kiukweli mechi ilikuwa nzuri sana kwa pande zote mbili ila safu yetu ya ulinzi ilikuwa imara na kuwadhibiti vizuri washambuliaji wa Stand ambao walishindwa kufika golini kwetu na kumfanya kipa wangu Owen Chauma kutokuwa na kazi kubwa ya kudaka maana mipira ilifika mara chache tena isiyokuwa na madhara," alisema Phiri

Kipindi cha pili Stand iliyochini ya Mfaransa Patrick Liewig iliamka na kujaribu kufanya mashambuliazi ambayo hayakuwa na madhara yoyote kwa Mbeya City na kujikuta wanamaliza mchezo wakiwa wameambulia pointi moja zilizowafanya wafikishe pointi 16 na kuendelea kushika nafasi ya pili nyuma ya Simba yenye pointi 17.

Akiizungumzia Simba, Phiri alisema kuwa, "Simba ni timu kubwa na ninafahamu uchezaji wao hivyo tunajiandaa kwani hata sisi tunahitaji pointi tatu kutoka kwao, hivyo waje tu,"

Mechi nyingine Kagera Sugar imekubali kichapo nyumbani cha mabao 2-0 toka kwa Toto African toka jijini Mwanza meci hiyo imechezwa uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Post a Comment

 
Top