BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, aliyekuwa Mbeya
KOCHA wa Mbeya City hapendi ujinga. Alimwambia beki wake John Kabanda kuwa akiingia uwanjani kazi yake kubwa iwe ni kumdhibiti Shiza Kichuya na baada ya kuona hajafuata maelekezo hayo aliamua kumtoa nje huku tayari winga huyo akiwa ameifungia timu yake bao.

Kichuya alifunga bao la pili la Simba huku la kwanza likifungwa na Ibrahim Ajib katika mechi iliyochezwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Akizungumza na BOIPLUS, Phiri alisema kuwa kabla ya mechi alizungumza na wachezaji wake na kuwapa tahadhari ya mchezaji mmoja mmoja wa Simba lakini hasa msisitizo ulikuwa kwa winga huyo mwenye kasi kubwa awapo na mpira.

"Ndiyo maana nilimtoa Kabanda alishindwa kumkaba Kichuya kama nilivyomuelekeza nilipofanya mabadiliko kidogo yalizaa matunda kwani kasi ya Kichuya ilipungua ingawa tayari alikuwa amefanya madhara ya kutufunga kipindi cha kwanza.

"Simba msimu huu iko vizuri na ndio maana ukicheza nao unatakiwa kuwa makini sisi walituwahi kipindi cha kwanza ila na mimi ilinigharimu kwani washambuliaji wangu hawana uwezo wa kumalizia wanapokuwa kwenye nafasi ya kufunga ni tatizo ambalo nitalifanyia kazi wakati wa usajili wa dirisha dogo," alisema Phiri.

Mbeya City inajiandaa na mechi dhidi ya Ruvu Shooting huku ikimkosa beki wake Rajab Zahir ambaye ana kadi tatu za njano na ikielezwa kwamba beki Haruna Shamte naye bado afya yake haijaimarika vizuri ambapo mechi iliyopita aliikosa.

Post a Comment

 
Top