BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
ALIYEKUWA Kocha wa Yanga Mholanzi Hans Pluijm leo alikuwepo uwanjani akishudia mabingwa hao wakiwambaratisha Maafande wa JKT Ruvu mabao 4-0 katika mechi ya kiporo ya ligi kuu ya Vodacom iliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.

Pluijm alijiuzulu juzi Jumatatu kuwafundisha mabingwa hao na kumwacha msaidizi wake Juma Mwambusi mpaka atakapopatikana Kocha mpya kwa mujibu wa Uongozi wa Yanga huku akishangilia muda wote wachezaji wa Yanga walipokuwa wakifanya vizuri hali iliyoashiria kuwa bado ana mapenzi na timu hiyo.

Mchezo huo ulihudhuriwa na mashabiki wachache kulinganisha na mechi zilizopita hali inayotafsiriwa huenda kitendo cha Kocha Hans kujiuzulu hakikuwafurahisha wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo.

Obrey Chirwa alipatia Yanga bao la uongozi dakika ya sita baada ya kupokea krosi ya Simon Msuva iliyoonekana kama haina madhara ambapo mabeki wa Maafande hao waliuacha mpira kabla ya kumkuta Mzimbabwe huyo akiwa na golikipa Saidi Kipao.

Amissi Tambwe aliyetokea benchi aliongeza bao la pili dakika ya dakika ya 63 baada ya kuichambua safu ya ulinzi ya Ruvu kabla ya Msuva kufunga la tatu zikiwa zimesalia dakika sita mtanange huo umalizike.


Beki Michael Aidan alifanya makosa ya kuchelewa kuokoa mpira dakika ya mwisho na kumuacha Tambwe akifunga bao rahisi la nne na kuzikata kabisa ngebe za Maafande hao.

Katika michezo miwili ya mwisho Yanga imefunga mabao 10 kitu kinachoweza kuwa mtaji mkubwa baadae endapo ligi hiyo itaamuliwa kwa idadi ya mabao huku wakifikisha alama 24 na kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Mwamuzi Elly Sasii aliwaonya kwa kadi ya njano wachezaji Kassim Kisengo,Nashon Naftal na Nurdin Mohamed kwa upande wa Ruvu na Kelvin Yondani kwa Yanga kutokana na mchezo usio wa kiungwana.

Post a Comment

 
Top