BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
LIGI Kuu ya Vodacom imeonyesha upinzani mkubwa lakini mwenendo wa Prisons ni wa kusuasua tu tofauti na msimu uliopita huku ikielezwa kwamba mwenendo huo unawashawishi viongozi wa Prisons kuanza kusaka kocha mpya hasa mzunguko wa pili baada ya Meja mstaafu Abdul Mingange kumaliza mkataba wake wa miezi sita.

Mingange amewahi kuifundisha timu ya Mbeya City lakini matokeo hayakuwa mazuri kiasi kwamba timu hiyo ilitaka kushuka daraja na ndipo walipomwajiri Mmalawi, Kinnah Phiri aliyenusuru hatari hiyo na baadaye Mingange alikwenda Ndanda FC ambako pia hakufanya vizuri, hivyo historia yake inaweza ikawa inamhukumu kutoongezwa mkataba na Maafande hao.

Habari ambazo BOIPLUS imezipata ni kwamba uongozi wa Prisons umefanya mazungumzo ya awali na kocha msaidizi wa Stand United, Athuman Bilali 'Bilo' ambaye pia amekiri kuwepo kwa mazungumzo hayo ingawa bado ana ajira na Wapiga Debe wa Shinyanga wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 16.

Prisons yenyewe ipo jijini Dar es Salaam ikijiandaa na mechi yao dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa uwanja wa Mabatini huku wakiwa wamekusanya pointi tisa pekee kutokana na mechi saba walizocheza wakati JKT Ruvu wao wana pointi saba na wamecheza mechi saba ambazo zimewaweka nafasi ya 14.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Prisons kilisema kwamba; "Mingange ana mkataba wa miezi sita na matokeo sio mazuri ingawa hatujacheza mechi nyingi, kiwango cha timu hakiridhishi hivyo kuna mazungumzo ambayo yanaendelea na Bilal wakikubaliana basi wakati wa mapumzo watafanya mabadiliko ya kocha."

Akithibisha hilo, Bilal alisema; "Ni mazungumzo tu yamefanywa ila hatujafikia makubaliano, hatua niliyofikia natamani kweli kuwa kocha mkuu kwani nina sifa hiyo, haya ni maisha hivyo nitawasikilizia kama kweli walikuwa na nia, timu yetu ya Stand imefikia mahali pazuri natamani imalize nafasi hii ya pili kwani itakuwa imetujengea sifa kubwa kwetu."

Mbali na Maafande hao lakini kuna habari kuwa Bilal pia anasakwa na Toto Africans ya jijini Mwanza ambayo sasa haina kocha mkuu baada ya Rogasian Kaijage kubwaga manyanga hivi karibuni, Bilali alikiri pia kuwepo kwa taarifa hizo.

Post a Comment

 
Top