BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
BENCHI la Ufundi la Yanga limetoa ufafanuzi wa kutowatumia  baadhi ya nyota wao katika michezo ya siku za karibuni wakiwemo Haruna Niyonzima na Vincent Bossou kwamba ni kutokana na sababu mbalimbali zinazowakabili wachezaji hao.

Niyonzima amecheza mechi chache msimu huu huku mara nyingi akitumika kama mchezaji wa akiba hali inayoleta sintofahamu kwa wapenzi wa mabingwa hao wanaodhani hakuna mahusiano mazuri kati yake na benchi hilo huku Bossou akikosekana katika michezo miwili.

Kocha Msaidizi wa mabingwa hao Juma Mwambusi ameiambia BOIPLUS kuwa kukosekana kwa wachezaji hao kunatokana na sababu tofauti ambapo Bossou ni mgonjwa tangu arejee kutoka Togo alipokuwa akiitumikia timu yake ya Taifa na Niyonzima hajapangwa kutokana kutoliridhisha benchi la ufundi ila bado ni mtu muhimu ndani ya kikosi.


"Bossou ni mgonjwa tangu arejee, afya yake haikutengemaa na kuhusu Niyonzima ni kwamba Yanga imesajili wachezaji wengi kwahiyo kuhusu kucheza ni suala la benchi la ufundi kuamua kutokana na kiwango cha mchezaji, kama hakucheza mechi zilizopita basi atacheza mechi zijazo kwani  bado ni mwajiriwa wa Yanga," alisema Mwambusi.

Mwambusi pia hakusita kutoa ya moyoni kuhusu upangaji wa ratiba kuwa inaziumiza timu kusafiri umbali mrefu kwenda mkoa ambao una timu zaidi ya moja badala ya kumaliza zote inacheza moja halafu inarudi tena kabla ya kwenda tena kitu kinachowachosha wachezaji na kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

"Ratiba ni changamoto kubwa Bodi ya Ligi  inapaswa kuangalia upya upangaji wa ratiba maana wachezaji wanachoka kiasi cha kushindwa kufanya vizuri uwanjani," alisema Mwambusi.

Post a Comment

 
Top