BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda
STRAIKA wa KRC Genk ya Ubelgiji na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ameonyesha kusikitishwa na sintofahamu inayoendelea kuhusu uhamisho wa winga wa Azam FC, Farid Mussa kwenda nchini Hispania katika klabu ya Teneriffe.

Farid alikwenda kufanya majaribio katika klabu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini humo na kufanikiwa kufuzu huku ikielezwa kilichokuwa kikisubiriwa ni kibali cha kufanya kazi nchini humo jambo ambalo limechukua muda mrefu hadi kuzua hofu miongoni mwa wadau wa soka nchini.

Samatta ambaye mara kadhaa amekuwa akikiri uwezo wa Farid ameandika katika ukurasa wake wa Istagram kuhusu hofu yake juu ya hatma ya kinda huyo huku akitaka kujibiwa ni nini hasa kinamkwamisha kwenda Hispania kuanza kazi.

"Taarifa zilizopo ni kwamba bado yupo Tanzania, kwanini yupo Tanzania wakati kila kitu kilishakwisha?, nani ana jibu la swali hili?, tafadhali, kuna nini nyuma ya pazia?," ilimaliza sehemu ya ujumbe huo mzito wa Samatta.

Katika ujumbe huo pia Samatta alielezea furaha aliyokuwanayo baada ya kusikia Farid amefuzu majaribio kwavile imani yake ni kwamba watanzania wengi wakipata timu nje ya nchi basi Stars pia itakuwa bora.

Farid aliondolewa kwenye kikosi cha Azam kinachoshiriki michuano ya Ligi Kuu kwa maelezo kuwa angeondoka muda wowote, lakini hadi sasa haifahamiki ataondoka lini licha ya viongozi wa Azam kusema zoezi la upatikanaji wa kibali cha kufanyia kazi nchini Hispania liko ukingoni.

Post a Comment

 
Top