BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SERIKALI imeagiza kusitishwa michakato yote inayoendelea ya kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwa Wanachama kwenda katika umiliki wa hisa na ukodishwaji kwa Klabu za Simba na Yanga hadi kutakapofanyika marekebisho ya katiba zao.

Katibu mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja amewaambia Waandishi wa Habari kuwa klabu hizo zinapaswa kurekebisha katiba zao kwanza kabla ya kufanya mabadiliko hayo kwa mujibu wa Sheria ya Baraza hilo na Kanuni za Msajili namba 442 Kanuni 11 kifungu kidogo cha (1-9) .

Kiganja alisema kuwa mabadiliko hayo yanayoendelea kwenye Klabu hizo tayari yameingia dosari baada ya baadhi ya Wanachama kwenda Mahakamani kupinga michakato hiyo kitu ambacho sio kizuri na pia sio ishara nzuri endapo yataachwa yaendelee.

"Tumesitisha michakato yote ya kubadili umiliki kutoka kwa Wanachama kwenda kwa uwekezaji kwa timu za Simba na Yanga mpaka watakapo fanya mabadiliko kwa mujibu wa Katiba za Klabu zao," alisema Kiganja.

Aidha BMT imemtaka mdau au mwanachama yoyote anayetaka kufanya uwekezaji kwenye Klabu hizo ni vema angeanzisha timu yake kama Saidi Salum Bakhresa alivyoanzisha Azam FC ili kupunguza malalamiko kwavile timu hizo zina Wanachama wengi.

Kiganja alisema kuwa michakato hiyo ilitakiwa ianzie kwenye matawi nchi nzima ili maamuzi yawe ya wote kwani mabadiliko yoyote ndani ya klabu hizo lazima yafuate Katiba zao.

Post a Comment

 
Top