BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
BEKI wa Mbeya City, Haruna Shamte amerejea kikosini baada ya kukosa mechi kadhaa akiwa majeruhi huku nyota watatu Ayoub Semtawa, John Kabanda na Omary Ramadhan wakikosa mechi ya kesho Jumamosi dhidi ya Majimaji itakayochezwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Nyota hao ambao wamecheza mechi zilizopita wanasumbuliwa na majeraha mbalimbali hivyo wameamua kuwapumzisha ili waendelee na matibabu chini ya uangalizi wa Daktari wao, Kaseko.

Ofisa Habari wa Mbeya City, Dismas Ten amesema "Wachezaji hao hawajapona majeraha yao waliyoyapata kwenye michezo yetu iliyopita, kulikuwa na dalili ya kupona kwa Omary lakini taarifa ya mwisho ndiyo hiyo kuwa hakuna uwezekano huo kwa sasa,”.

Semtawa aliumia wakati timu hiyo ilipocheza na African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru na atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu ina maana kwamba atakosa mechi zote tatu zilizobaki za mzunguko huu wa kwanza wa ligi wakati Kabanda na Omary wanaweza kurejea uwanjani mechi ijayo dhidi ya Yanga itakayochezwa Novemba 2 uwanja wa Sokoine.

Kocha Kinnah Phiri alisema wachezaji wake wako vizuri ingawa anaona kutakuwa na upinzani mkubwa kutokana na kwamba timu zote zinahitaji matokeo mazuri "Lazima tuhakikishe tunapata matokeo mazuri ili hesabu zangu zisiharibike katika raundi hii ya kwanza, hivyo tutapambana kuwadhibiti wapinzani wetu,".

Post a Comment

 
Top