BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SASA inaonekana timu ya Simba imeamua kuchukua ubingwa msimu huu kwa mtindo wowote baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo kutokana na matokeo mazuri wanayoyapata kwenye mechi zake za ligi ya Vodacom inayoendelea.

Simba imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC na kuendelea kujikita kileleni mwa ligi kuu baada ya kufikisha alama 26 katika michezo 10 iliyoshuka dimbani mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Simba walianza kwa kasi zaidi kwa kulishambulia lango la Mbao kama nyuki lakini vijana wa Kocha Ettiene Ndaliyajage walikuwa imara zaidi kuanzia kiungo hadi ulinzi na kuwafanya Wekundu hao kwenda mapumziko bila kupata bao.

Kipa wa Mbao Emmanuel Mseja aliokoa michomo kadhaa iliyokuwa ikielekea wavuni ambapo dakika ya 14 alipangua shuti la Laudit Mavugo kabla ya kuokoa michomo mingine dakika za 24 na 32.

Kuingia kwa mshambuliaji Fredrick Blagnon kuliongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Simba lakini bado walinzi wa Mbao walikuwa makini kuhakikisha nyavu zao hazitikiswi kwa namna yoyote.

Kiungo Muzamiru Yassin aliifungia Simba bao la ushindi dakika ya 86 baada ya kupokea pasi safi ya kichwa toka kwa Blagnon na kuingia ndani ya eneo la hatari akiwa peke yake bila upinzani wowote kutoka kwa Wachezaji wa Mbao na kuuweka mpira nyavuni.

Simba iliwatoa Mavugo na Ibrahim Ajib nafasi zao zikachukuliwa na Blagnon pamoja na Mohamed Ibrahim huku Mbao ikiwatoa mkongwe Hussein Swedi na Pius Buswita na kuwaingiza Boniface Maganga na Frenk Damas.

Post a Comment

 
Top