BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Shinyanga
KIUNGO Mohamed Ibrahim 'MO' ameonyesha sababu ya Kocha Joseph Omog kumuamini na kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza baada ya leo kuonyesha kiwango cha hali ya juu Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage.

MO ambaye amesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar alikuwa hapangwi katika mechi za mwanzoni mwa ligi lakini baada ya kupewa nafasi ya kucheza katika michezo ya hivi karibuni amekuwa na mchango mkubwa kwa Wekundu hao.

Kiungo huyo alifunga mabao mawili katika dakika za 32 na 50 huku akisaidia upatikanaji wa jingine lililofungwa na Shiza Kichuya dakika ya 45 wakati huo akionesha kandanda safi kwa muda wote wa mchezo kwa kutoa pasi za uhakika kwa wachezaji wenzake.


Mshambuliaji Laudit Mavugo alitolewa dakika ya 42 baada ya kutokuwa mchezoni kutokana na kukosa nafasi kadhaa za wazi na nafasi yake kuchukuliwa na Ame Ally 'Zungu' ambaye alisaidia kupatikana kwa bao la tatu lililofungwa na MO.

Pamoja na ushindi huo wa mabao 3 bado Simba waliendelea kucheza vizuri huku wakionekana kama wapo nyumbani baada ya kutawala sana mchezo huo hasa kipindi cha pili ambapo Mwadui hawakuwa mchezoni na endapo Wekundu hao wangeongeza umakini wangepata mabao mengi zaidi.

Simba wameendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 32 baada ya kushuka dimbani mara 12 huku wakioneka wana dhamira ya kweli ya kunyakua ubingwa msimu huu.

Matokeo mengine ya mechi za leo
African Lyon 1-1 Tanzania Prisons
Toto African 3-2 Mtibwa Sugar
Mbeya City 3-2 Majimaji
JKT Ruvu  1-0 Ndanda FC

Post a Comment

 
Top