BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Shinyanga
STAND United wamewasili mchana wa leo Jumatatu mjini Shinyanga wakitokea Pwani ambako walikuwa na mechi dhidi ya Ruvu Shooting na keshokutwa Jumatano watacheza na Simba ambayo tayari ipo mjini hapa ila wametamka kuwa hawajachoka bado wana nguvu za kuwavaa wapinzani wao na kushinda.

Mbali na hayo, Stand United wameenda mbali kimtazamo kwamba wanajuwa Simba wanacheza na ratiba kwani inawapa nafasi ya kupumzika ila wao watacheza na dakika 90 za uwanjani kwani ratiba ya mechi zao imekuwa ikiwabana na kucheza pasipo kupumzika tofauti na Simba ambao wamecheza mechi mbili sehemu moja.

Stand jana Jumapili walikuwa uwanja wa Mabatini na baada ya mechi hiyo walilazimika kuanza safari ili kuwahi mapumziko ya saa chache kabla ya kuingia tena uwanjani. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa CCM Kambarage.

Kocha wa timu hiyo, Athuman Bilali ameiambia BOIPLUS kuwa, "Ukweli ni kwamba tumeingia mchana kwenye saa nane kasoro hivi na baadaye tulikwenda kupasha kwenye Uwanja wa Mwasele, tunajuwa wenzetu wapo hapa hapa ila tunawaambia hivi sisi hatujachoka tupo tayari kucheza nao na kuwafunga,".


Bilali alisema kuwa pamoja na changamoto wanazozipata ila wanaamini mambo yao yatakuwa mazuri na ndio maana wanapambana ili kuwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi kuu.

Mwenyekiti wa klabu ya Stand United, Dr Ellyson Maeja alisema kuwa, "Ni kwamba Simba wanacheza na ratiba ila sisi tutacheza uwanjani kwa dakika 90, vijana wetu wameingia tangu mchana, wamesafiri umbali mrefu hawajakata tamaa katika mapambano haya, tuna hali ngumu lakini bado wanapigana na uwezo wa kuwafunga Simba walioshikilia ratiba tunao,".

Mechi iliyopita Stand wanaoshika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 22 walitoka sare tasa na Ruvu Shooting wakati Simba wanaoongoza ligi kwa kukusanya pointi 32 waliifunga Mwadui bao 3-0 mechi iliyochezwa Uwanja wa CCM Kambarage mjini hapa.

Post a Comment

 
Top