BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SIKU moja baada ya Serikali kusitisha mchakato wa uendeshwaji wa timu kutoka kwa Wanachama kwenda katika mfumo wa hisa na ukodishwaji, Uongozi wa Klabu ya Simba umesema unasubiri barua rasmi kutoka Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ili watoe msimamo wao.

Katibu mkuu wa Klabu ya Simba Patrick Kahemele ameiambia BOIPLUS kuwa wanasubiri barua rasmi kutoka BMT ili Kamati ya Utendaji iketi kujadili kabla ya kufikia maamuzi ambayo watayatangaza kwa Wanachama wote.

Wanachama wa Klabu ya Simba walishakubaliana kuhusu suala la uwekezaji ambapo mfanyabiashara Mohamed Dewji 'MO' amekubali kuwekeza hisa za asilimia 51 ambazo zingengamfanya kuwa na kauli ya mwisho katika masuala mbali mbali ya kiutendaji ndani ya klabu hiyo.

Kahemele alisema "Kwa sasa tunasubiri barua kutoka BMT na tutaitisha kikao cha Kamati ya Utendaji kujadili suala hilo, tutakachoafikiana tutawaambia Wanachama kwa sasa hatuwezi kutoa msimamo wetu."

Kwa upande wa Klabu ya Yanga BOIPLUS ilimtafuta Kaimu Katibu mkuu wao Baraka Deusdedit lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

Jana Katibu mkuu wa BMT Mohamed Kiganja aliagiza kusitishwa kwa michakato yote inayoendelea ya kubadili uendeshwaji kwa Klabu hizo kongwe mpaka watakapobadili katiba zao kwa mujibu wa Sheria ya Baraza Michezo la Taifa.

Post a Comment

 
Top