BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
UONGOZI wa Simba umeamua kuingia jukumu la kutengeneza viti vilivyovunjwa na mashabiki wao ili kukwepa gharama kubwa ambayo wangelipa moja kwa moja serikalini kama fidia ya uharibifu huo.

Mashabiki wa Simba walifanya uharibifu huo kwenye mechi yao na Yanga baada ya mwamuzi Martin Saanya kumpa kadi nyekundu Jonas Mkude huku akikubali goli la Amissi Tambwe lililodaiwa kuwa aliunawa mpira kabla hajafunga.

Serikali kupitia wizara yake ya Habari, Utamaduni na Michezo, ilifanya tathmini ya uharibifu huo na kubaini kwamba viti 1,781 viling'olewa na mashabiki waliodaiwa kuwa wa Simba ambapo gharama ya kiti kimoja ni Sh 100,000 na wangepaswa kulipa Sh 178 milioni.

Habari ambazo BOIPLUS imezipata ni kwamba uongozi wa Simba ulikutana na Waziri, Nape Nnauye na kuomba kutengeneza viti hivyo ambapo walikubaliwa kufanya kazi hiyo wenyewe ambayo inatarajia kuanza kesho Jumamosi baada ya leo wataalamu walikwenda kufanya ukaguzi.

"Simba wanatengeneza wenyewe vile viti na pesa ya kutengenezea ametoa kiongozi mmoja wa Simba (Jina tunalo) baada ya kukubaliwa na serikali maana wangeambiwa walipe fidia ni pesa nyingi sana ingewatoka kuliko kutengeneza wenyewe," kilisema chanzo hicho kutoka TFF.

Alipoulizwa Rais wa Simba, Evans Aveva alisema kuwa, "Ni kweli tunafanya marekebisho wenyewe na tulipanga kuanza leo, kila kitu kipo tayari bado kazi kuanza tu,".

BOIPLUS ilifika uwanjani hapo kushuhudia lakini walinzi waliokuwepo walikiri kufika kwa wataalamu watakaotengeneza viti hivyo na kwamba wameahidi kurejea kesho Jumamosi kwa ajili ya kuanza kazi rasmi.

Post a Comment

 
Top