BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
UONGOZI wa Klabu ya Simba umelilalamikia Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) kupitia Bodi ya ligi kwa kutokuwa makini katika kupanga waamuzi hasa kwenye mechi kubwa baina ya Simba na Yanga.

Katika mchezo wa watani hao uliofanyika Oktoba mosi mwamuzi Martin Saanya alipewa jukumu la kuchezesha ikiwa ndo mechi yake ya kwanza tangu alipofungiwa mwaka mmoja baada ya kuboronga msimu uliopita.

Ofisa Habari wa Simba Haji Manara alisema kuwa "haiwezekani kwa mwamuzi anatoka kufungiwa mwaka mmoja na anapewa kuchezesha mechi kubwa ya watani huko ni kukosekana kwa umakini kwa vyombo vinavyosimamia mpira wa nchi hii."

"Mwamuzi alishindwa kumudu mchezo kabisa, alikuwa anatoa maamuzi ambayo yalionekana dhahiri kuwa na faida upande wa pili hili ni suala ambalo linatakiwa kutazamwa kwa makini," alisema Manara.

Manara aliongeza pia kama kuna uwezekano waamuzi watakaochezesha mechi hizo watoke nje ya nchi na isiwe hizi za Afrika Mashariki na kati ili matokeo yatokane na uhalisia kwakua kila mara kutakuwa kunatokea matukio ya uvunjifu wa amani.

"Sio mbaya waamuzi kutoka nje na hata kama ni gharama za kuwalipa sisi tuko tayari kutoa. Ni bora kumlipa mwamuzi kutoka nje pesa nyingi kuliko kutoa pesa za ukarabati na faini ambazo zinasababishwa na watu wachache".

"Wenzetu Misri wanafanya hivyo, mechi ya Al Ahly na Zamalek waamuzi wanatoka nje ili kuondoa shaka ya matokeo ya mchezo siyo mbaya nasi tukaiga hiyo" alisema Manara.

Wakati huo huo Manara alisema kikosi cha timu hiyo kinatarajia kuondoka wikiendi ijayo kuelekea jijini Mbeya tayari kwa mchezo wao dhidi ya Mbeya City Jumatano ijayo.

Post a Comment

 
Top