BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
UONGOZI wa Klabu ya Simba umesema utaangalia marudio ya mchezo wao dhidi ya Yanga kupitia mkanda wa video ili kujiridhisha na maamuzi ya refarii Martin Saanya kabla ya kutoa maamuzi mazito.

Simba inaamini mwamuzi huyo ndiyo chanzo cha vurugu baada ya kukubali goli la Yanga ambalo mfungaji Amissi Tambwe aliushika mpira mbele ya mwamuzi kitu kilichopelekea kutokea vurugu hadi kufikia mashabiki wanaoaminika kuwa ni wa Simba kung'oa viti vya uwanja.

Ofisa Habari wa klabu hiyo Haji Manara alisema hawajaridhishwa na maamuzi ya Saanya ya kukubali goli la Tambwe na kumzawadia nahodha wao kadi nyekundu ambapo wataangalia marudio ya mchezo huo kabla ya kuchukua hatua stahiki.

Manara alitamka wazi wazi kuwa mara zote wanapocheza na watani wao Yanga lazima ipatikane kadi nyekundu upande wao ambayo inaonekana dhahiri ni kwa ajili ya kuwabeba mabingwa hao.

"Tunaenda kutazama mchezo wote kupitia mkanda wa video na tukibaini tumehujumiwa hatutakubali kwakua wamezidi kutuonea," alisema Manara.

Aidha Manara alisema pia uongozi umepinga vikali vurugu zilizojitokeza baada ya mashabiki wake kufanya fujo kutokana na kutoridhishwa na maamuzi ya refarii.

"Tumesikitishwa na vurugu zilizojitokeza na hatuungi mkono hata kidogo kwakua zilizoharibika ni mali za umma ila chanzo ni mwamuzi," alimalizia Manara.

Post a Comment

 
Top