BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SERIKALI imezipiga marufuku timu za Simba na Yanga kutumia uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa muda usiojulikana baada ya ghasia zilizojitokeza katika mchezo wao wa jana.

Ghasia hizo ni pamoja na kuvunja mageti manne ya kuingilia uwanjani pamoja na viti 1781 vilivyoharibiwa na mashabiki wa Simba ambao hawakuridhishwa na maamuzi ya refarii Martin Saanya.

Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye alitembelea uwanja huo kushuhudia hasara iliyotokea ambapo alisema kuwa kutokana na vurugu hizo Serikali imeamua kuzifungia timu hizo kwa muda usiojulikana kutumia uwanja.

"Tumezifungia Simba na Yanga kutumia uwanja wa Taifa kwa muda usiojulikana kutokana na vurugu zilizojitokeza ili iwe fundisho," alisema Nape.

Waziri huyo pia alisema mapato ya mchezo huo hayatagawanywa kwa klabu hizo hadi itakapofahamika ni kiasi gani kinahitajika kukarabati miundombinu ya uwanja huo na endapo fedha hizo hazitatosha basi italazimika timu hizo kuongeza ili kufidia.

Aidha Waziri Nape alisema kutafungwa kamera maalum kwa ajili ya kuonesha mashabiki wote walioingia uwanjani hapo ili kuwashughulikia wale watakaofanya vurugu za aina yoyote.

Wakati huo huo Nape alisema mfumo wa tiketi za Kielektroniki ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa baada ya kuingiza mashabiki 43,000 idadi ambayo ni kubwa huku ikiwa ndiyo mara ya kwanza kutumika tena katika mechi kubwa.

Katika mchezo huo miamba hiyo ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 huku ikishuhudiwa Simba wakicheza pungufu baada ya nahodha Jonas Mkude kulimwa kadi nyekundu.

Post a Comment

 
Top