BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
BAADA ya timu za Simba na Yanga kufungiwa na Serikali kutumia Uwanja wa Taifa kutokana na vurugu za mashabiki wao walizofanya Oktoba mosi vigogo hao wa soka nchini wamesema hata   Uwanja wa Uhuru 'Shamba la bibi' ni poa tu kikubwa ni ushindi.

Timu hizo zimehamia Uwanja huo wenye nyasi bandia ambapo awali waliukataa kutokana na kusababisha majeruhi kwa wachezaji wao na Simba waliliandikia barua Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) kuupinga kutokana na uchakavu wa eneo la kuchezea lakini baada ya kupigwa marufuku kutumia Uwanja wa Taifa sasa hawana chaguo, wamekubali yaishe.

Meneja wa Simba Mussa Mgosi ameiambia BOIPLUS kuwa kwa sasa hawachagui Uwanja, wapo tayari kucheza popote kwavile mikoani kuna viwanja vibovu kuliko hata Shamba la bibi huku wakijipanga kuhakikisha wanaibuka na pointi zote tatu watakaposhuka katika dimba lolote.

"Sisi popote pale tunacheza hata wakitupeleka Karume tupo tayari kikubwa ni kuhakikisha tunashinda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuchukua ubingwa msimu huu," alisema Mgosi.

Mgosi aliongeza kuwa Wekundu hao wanaoongoza ligi wakiwa na pointi 23 wameingia kambini leo kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wao dhidi ya Mbao FC utakaopigwa keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru baada ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa upande wao Yanga kupitia kwa Kocha wao msaidizi Juma Mwambusi alisema kuwa wapo tayari kucheza Uwanja wowote watakaopangiwa kucheza na hawahofii chochote kwakua wana kikosi bora chenye uwezo wa kucheza na timu yoyote nchini huku wakiwa mabingwa watetezi kwahiyo suala la Uwanja wa Uhuru haliwaumizi kichwa.

"Uwanja wa Uhuru sio mbaya na kwavile ndiyo tumepangiwa kuutumia basi hatuna jinsi na hata ingekuwa sehemu nyingine tupo tayari kikubwa ni kuibuka na pointi tatu, tumejipanga kupambana popote," alisema Mwambusi.

Post a Comment

 
Top