BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
SIKU chache baada ya Serikali kuzifungia Simba na Yanga  kutumia  uwanja wa taifa,Viongozi wa timu hizo jana wamekutana na Wizara ya Habari  Sanaa Utamaduni na Michezo na ili kuomba kupunguziwa adhabu hiyo ikiwezekana  warejeshwe kutumia dimba hilo.

Jumapili iliyopita Waziri mwenye dhamana ya Michezo Nape Nnauye alitembelea uwanja huo kujiridhisha na uharibifu uliojitokeza kabla ya kutoa tamko kwa niaba ya Serikali ya kuzifungia timu hizo kongwe nchini ili kukomesha kadhia hiyo.

Kiongozi mmoja wa Simba ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwenye mtandao huu ameiambia BOIPLUS kuwa  wamekubaliana na Serikali kufanya ukarabati wa uwanja huo ambapo viti 1781 vilivunjwa na mashabiki wa Simba baada ya Mwamuzi Martin Saanya kukubali bao la utata la Amissi Tambwe pamoja na kadi nyekundu ya Jonas Mkude.

"Wamekubali ombi letu na kufanya ukarabati wa uharibifu uliojitokeza tupo tayari kwa kila kitu watakachosema tufanye ili tuendelee kutumia uwanja huo ambao umekuwa ukituingizia mapato makubwa," alisema Kiongozi hiyo.


Wakati huo kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusdedit amemuandikia barua Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kuomba kutumia uwanja wa Amani kwa ajili ya mechi zake za ligi baada ya kupigwa marufuku uwanja wa Taifa.

Endapo Yanga watakubaliwa ombi lao basi tutashuhudia historia nyingine ikiandikwa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara ikichezwa pia Visiwani Zanzibar.

Post a Comment

 
Top