BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally. Mbeya
LICHA ya kuwepo na changamoto ya tiketi chache zilizotumwa na Bodi ya Ligi ambao ni wasimamizi wa ligi kuu Bara lakini mechi ya Mbeya City na Simba imeingiza Sh 60 milioni tofauti na msimu uliopita ambapo msimu mzima hakuna mechi iliyoingiza kiasi kikubwa cha fedha kama mechi ya jana.

Katika uwanja wa Sokoine ambao ulitumika kwa mechi hiyo iliyoingiza mashabiki 11255 kulikuwa na changamoto ya tiketi ambazo zilimazilika mapema kwani Bodi ya Ligi ilituma tiketi 5,000 wakati uwanja huo unaingiza mashabiki kati ya 20,000 hadi 25,000.

Hata hivyo chama cha soka mkoa wa Mbeya na wasimamizi wa mechi hiyo walifanya jitihada za kupata tiketi nyingine za ziada ambapo walilazimika kuuza vishina 5,000 vya tiketi za jana na vishina vingine 5,000 vya mechi zilizopita ili kuokoa jahazi hilo.

Katika mgao huo Simba ambayo iliingiza asilimia kubwa ya mashabiki ilipata Sh 9.9 milioni wakati Mbeya City ambao ni wenyeji walipata Sh 19.9 milioni huku ikidaiwa msimu uliopita mapato ya juu yalikuwa ni mechi dhidi ya Yanga na Mbeya City iliyoingiza Sh 50 milioni.

Akizungumza na BOIPLUS msimamizi wa mechi hiyo, Haroub Seleman alisema kuwa walikamata tiketi 34 ambazo zilinunuliwa na walanguzi waliokuwa wanauza tiketi moja ya sh 7,000 kwa Sh 10,000 na tayari Jeshi la Polisi linaendelea kuchukuwa hatua za kisheria kwa walanguzi hao.

"Hizo ni zile chache tu tulizofanikiwa kuzikamata ila nyingi walikuwa wameuza, tiketi zililetwa chache ikidhaniwa kwamba mechi haitakuwa na mashabiki wengi kwani siku za hivi karibuni mashabiki waliacha kuingia uwanjani na badala yake wanaangalia mechi kwenye televisheni.

"Lakini tulipambana kupata suluhusho na ndio maana mashabiki wengi waliingia na vile vishina vilibaki, tumejifunza na hili halitajirudia kwenye mechi kubwa kama hizi," alisema Haroub.

Post a Comment

 
Top