BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
TIMU ya Zesco United ya Zambia imesema haitambui kitu chochote kinachoendelea kuhusu Kocha wao mkuu George Lwandamina kuwepo nchini Tanzania kusaini mkataba wa miaka miwili kuwafundisha mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Vodacom, Yanga.

Lwandamina ana mkataba wa miaka mitatu ambao utafikia kikomo Januari 2017 na hakuna majadiliano yoyote ya kuongeza mkataba na Kocha huyo hajazungumza chochote na Uongozi na Zesco kama anataka kuiacha klabu hiyo.

Kwamujibu wa Kaimu Katibu mkuu wa Klabu hiyo Richard Mulenga alisema Lwandamina aliaga anaenda kwenye maombolezo ya msiba wa ndugu yake aliyefariki dunia na alipewa ruhusa na Meneja wa timu Mabvuto Banda kuanzia siku ya Jumapili na alitarajiwa kuripoti kambini usiku wa leo kwa ajili ya kupanga kikosi kitakachoshuka dimbani kesho dhidi ya Nkwazi FC mjini Lusaka.

Uongozi wa Zesco unasema endapo taarifa hizo za vyombo vya Habari zitakuwa ni za kweli basi Kocha huyo atakuwa amevunja mkataba nao kitu ambacho hawakukitarajia kutokea hasa kwa mtu mwenye uweledi kama Lwandamina.

Zesco wamekuwa wakipata taarifa kutoka kwenye vyombo vya Habari mbalimbali nchini Tanzania na Zambia kuwa Kocha wao amesaini mkataba wa miaka miwili na Yanga bila kufanya mazungumzo yoyote na Uongozi wa Klabu hiyo kitu kinachotafsiriwa kuwa ni kuvunja mkataba.

Taarifa ambazo BOIPLUS imezipata ni kwamba Kocha huyo anatarajiwa kuanza kukinoa kikosi cha Yanga Novemba Mosi baada ya taratibu zote kukamilika.

Post a Comment

 
Top