BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
MSANII wa muziki wa kizazi kipya Hamadi Ally 'Madee' amesikitishwa na kitendo cha timu yake ya Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1 na watani wao wa jadi Simba licha ya kuwa pungufu uwanjani kwa muda mrefu. 

Katika mchezo huo Simba ilisawazisha bao dakika ya 86 kupitia kwa winga Shiza Kichuya huku wakiwa pungufu baada ya nahodha wao Jonas Mkude kuoneshwa kadi nyekundu katikati ya kipindi cha kwanza.

Madee ambae  ni kiongozi wa kundi la Tip Top connection ambalo linafanya vizuri katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya alisema timu yake ya Yanga ilistahili kuibuka na ushindi lakini wachezaji waliridhika na goli moja kabla ya wapinzani kusawazisha.

Akizungumza na BOIPLUS Madee alisema  Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri na matokeo ya sare waliyoyapata jana bado hayawafanyi kushindwa kutetea taji lao la ubingwa walilolipata misimu miwili mfululizo. 

"Tuna kikosi kizuri, hatuwezi kukata tamaa bado tuna mechi nyingine ambazo tunaweza kucheza na kupata matokeo mazuri na tukarejea katika nafasi yetu," alisema Madee.

Madee maarufu kama Rais wa manzense alisema yeye ni shabiki nambari moja wa Yanga na  anaamini bado msimu huu wanayo nafasi ya kutetea ubingwa kutokana na ubora wa kikosi chao ambacho kimekaa pamoja muda mrefu kulinganisha na timu nyingine.

Post a Comment

 
Top