BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
WIKI iliyopita Mwamuzi, Thomas Mkombozi alipokea kipigo kutoka kwa mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa Coastal Union baada ya kutoa penati kwa KMC zilipokutana  katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iliyomalizika kwa wageni kuibuka na ushindi wa mabao 3-2, unajua kasemaje?, yeye kidume, hawezi kuacha kuchezesha na kwamba kipigo hicho hakimfanyi ashindwe kuifanyia kazi taaluma yake.

Mechi hiyo ilichezwa uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ambapo vurugu hizo zilipelekea mwamuzi huyo kuumizwa na kukimbizwa hospitali alikoshonwa nyuzi nne kisogoni na nyuzi moja sehemu ya usoni kutokana na mawe aliyokuwa akirushiwa na mashabiki hao.

Hata hivyo Mkombozi amesema kuwa hizo ni changamoto katika kazi na vurugu za mashabiki hao hazimkatishi tamaa kuwa aachane na fani yake hiyo aliyoisomea bali yeye ni mwanaume jasiri na ataendelea kupambana huku akiwataka mashabiki, viongozi kutambua kuwa katika mechi kuna kushinda na kupoteza mchezo.

"Kwanza nilijua kama ni utani ila ghafla nikaona hali imebadilika, mashabiki walizidi kurusha mawe kutokea pale jukwaani, ndipo hapo nikaona nianze kujihami kwa kupangua mawe na virungu vilivyokuwa vikirushwa kuja kwangu, ilikuwa hatari sana na tayari nimefungua kesi ya shambulio katika kituo cha Polisi Tanga ingawa tayari mimi nimerejea kwangu Moshi.

"Inasikitisha sana kuona mashabiki hata viongozi hawawezi kukubali matokeo ya mechi yao, ila nawaambia tu kuwa mimi sina uoga ni mwanaume jasiri, sitaacha taaluma yangu kwa vurugu hizi za mashabiki najua haki itatendeka kwani nimewasilisha taarifa sehemu sahihi, Polisi na TFF (Shirikisho la Soka nchini)," alisema Mkombozi ambaye pia ni askari Polisi.

Akizungumzia uzoefu wake, Mkombozi alisema; "Nimechezesha VPL tangu mwaka 2000 kwa maana hiyo nina miaka 16 sasa, nina uzoefu wa kutosha ila ndo hivyo kupangwa mechi za FDL lazima uwe na roho ngumu, watu hawataki kufungwa, mimi ni mwanaume jasiri ndiyo maana niliweza kupangua mawe na virungu vilivyorushwa kwangu,".

Vurugu hizo zilizotokea Jumamosi iliyopita zimepelekwa katika Kamati ya Masaa 72 ambayo hupaswa kutoa hukumu ndani ya masaa hayo kwa maana ya siku tatu lakini hadi sasa ni siku ya tano viongozi wa kamati hiyo wakisema kuwa wanaendelea kukusanya taarifa ndipo wakutane.

Post a Comment

 
Top