BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
SIMBA ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kufungwa na Stand United kwenye uwanja wa CCM Kambarage msimu uliopita wakafuata Yanga msimu huu, vigogo wote hao walipigwa bao 1-0 na saa wamesema ni zamu ya Azam FC.

Stand itawakaribisha matajiri hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Jumatano ijayo huku wakiwaambia kwamba ni lazima wafute uteja kwani hawajawahi kupata ushindi kwa Azam tangu wapande daraja kushiriki ligi kuu na mara zote wamekuwa wakipigwa nje ndani.

Stand hivi sasa wapo njiani kuelekea Shinyanga baada ya kuambulia sare tasa na Mbeya City ambapo wamekusanya pointi 16 zilizowaweka nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakitanguliwa na Simba wenye pointi 17 wakati Azam wao wana pointi 11 sawa na Yanga pamoja na Ndanda FC lakini Azam inashika nafasi ya saba, Yanga wanashika nafasi ya sita huku Ndanda anashika nafasi ya nane.

Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilali aliiambia BOIPLUS kuwa walishindwa kupata ushindi katika mechi yao iliyopita kwa kile alichokieleza kuwa kikosi chao kilicheza kwa kujilinda sana huku wakifanya mashambulizi machache.

"Unajuwa kucheza ugenini kuna mambo mengi sana hivyo ni lazima tujilinde ingawa tulishambulia mara chache bila mafanikio, tunarudi nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya mechi ijayo.

"Hatujawahi kuwafunga Azam tangu tupande daraja lakini msimu huu tumepania kufuta uteja kwa timu zote za Dar es Salaam, tulianza na Yanga sasa ni zamu ya Azam na hata hao Simba wakija nao lazima waache pointi tatu nyumbani," alisema Bilal.

Msimu huu Azam imekuwa na mwenendo usioridhisha ukilinganisha na msimu uliopita wakati Stand wao wakisisitiza kushinda mechi tano ili wajihakikishia kutoshushwa nafasi ya pili.

Post a Comment

 
Top