BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SHIRIKISHO la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limesema linaitambua Yanga kama klabu ya mpira inayoongozwa na Mwenyekiti Yusuph Manji na haitambui mabadiliko yoyote ya kiuendeshaji yaliyotokea siku za karibuni.

Wiki iliyopita Uongozi wa klabu hiyo ulitoa nakala ya mkataba iliyosaini kwa ajili ya kuikodisha kwa miaka 10 na kampuni ya Yanga Yetu inayomilikiwa na Mwenyekiti wake Yusuph Manji.

TFF imewataka mabingwa hao wa ligi kwa misimu miwili mfululizo kuwapelekea nakala ya mkataba huo walioingia na kampuni hiyo ili waupitie na kuangalia kama katiba na mlolongo mzima umefuatwa kabla ya kufikia hatua ya kusainiwa.

Katibu Mkuu wa TFF Celestine Mwesigwa aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa msimamo wa Shirikisho hilo ni kwamba hawatambui mabadiliko yoyote ya kiundeshwaji yaliyofanyika zaidi ya kuwa Yanga ni klabu ya Mpira kama ilivyosajiliwa kwa mujibu wa sheria.

"Tumewaagiza Yanga kutuletea nakala ya mkataba waliosaini na kampuni hiyo tuupitie kwakua TFF ndiyo chombo kinachoongoza mpira wa nchi hii," alisema Mwesigwa.

Mwesigwa alisema kama walivyowazuia kupitisha katiba mwezi wa sita kutokana na kuwa na mapungufu ambayo waliwataka kuyafanyia kazi ndiyo wameomba nakala ya mkataba huo ili kuupitia na  endapo utaonekana hauko vizuri pia watawataka waurekebishe kwa manufaa ya Yanga.

Katibu huyo alisema kuwa Yanga ina wanachama wengi na kuna wanaopinga mchakato huo na wanaokubali kwahiyo TFF lazima iingilie kati kabla ya mambo hayajaharibika zaidi.

"Tuliwaita awali watuelezee kuhusu hili muda mfupi baada ya kufanya mkutano mkuu wa dharura mwezi Juni lakini Katibu wao alitutaka tuongee na bodi ya wadhamini kitu ambacho hakipo kwa mujibu wa sheria," alisema Mwesigwa.

Post a Comment

 
Top