BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally & Akram Msangi, Mbeya
TIKETI za mechi ya Simba na Mbeya City ambayo itachezwa muda mfupi kuanzia sasa ziliisha huku kukitokea vurugu baada ya mashabiki kugundua kuwa kuna baadhi ya watu wamenunua tiketi nyingi na kuwauzia wengine kwa bei ya juu.

BOIPLUS ambayo ipo uwanjani hapa imeshuhudia mashabiki wakifanya vurugu wakishinikiza wauziwe tiketi hizo ambazo alizishika dada mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja. Baada ya kuona hivyo dada huyo alikimbia na kwenda kujificha kwenye kibanda cha mama ntilie kuokoa uhai wake mpaka polisi walipofika kumchukuwa.

Haikufahamika mara moja kuwa dada huyo alikusanya tiketi ngapi ila ilielezwa kuwa alinunua tiketi nyingi za Sh 7000 ambapo yeye alikuwa akiziuza kwa Sh 10,000 ambapo Polisi walimchukuwa kumpeleka kwenye chumba maalumu kilichopo ndani ya uwanja wa Sokoine kwa mahojiano zaidi.

Habari zaidi ambazo BOIPLUS imekusanya hapa uwanjani ni kwamba TFF ilileta tiketi 10,000 wakati uwanja unaingiza mashabiki kati ya 20,000 hadi 25,000.

Hata hivyo muda mfupi baadaye TFF kupitia chama cha soka mkoani hapa kiliagiza gari lingine lililoleta tiketi na hivyo mashabiki kuendelea kukata tiketi na kuingia uwanjani.

Post a Comment

 
Top