BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
WENGI wanadhani kuwa kasi ya Simba ilivyo sasa inaweza kuwapelekea Wekundu hao kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom msimu huu lakini straika wa zamani wa Yanga, Boniface Ambani amesema bado ligi ni changa na si rahisi kuipa Simba nafasi ya kutwaa ubingwa.

Ambani ambaye aliwahi kuwa Mfungaji Bora wa ligi hapa nchini ameiambia BOIPLUS kuwa hata Yanga ina nafasi ya kutetea ubingwa kama kocha Hans Pluijm ataamua kuwapumzisha wachezaji wake ambao wamecheza mechi nyingi mfululizo zikiwemo zile za michuano ya CAF.

"Nadhani wanachotakiwa kufanya Yanga ni kuwapumzisha wachezaji hasa ambao walitumika sana katika mashindano ya CAF, wangeanza kuwatumia baada ya mechi tano hivi.

"Wachezaji wa Yanga wamechoka sana na uchovu wao umekolea kwa hivyo wanaweza tetea taji lao lakini ni kwa kutumia  nguvu nyingi mno. Simba hawakuwa na presha yoyote, mpaka wafike huko mbele watakuwa wamekusanya pointi nyingi ila pia huwezi kusema watatwaa ubingwa maana ligi bado ni changa," alisema Ambani.

Ambani alisema kuwa katika soka mambo yanaweza kubadilika kwani aliyeanza vizuri anaweza kumaliza vibaya huku aliyeanza vibaya akamaliza vizuri na hiyo inaweza kutokea kwa Yanga kama kocha atakubali kuwatumia wachezaji ambao hawajacheza sana.

Simba ndiyo inayoongoza ligi ikiwa na pointi 23 na mechi moja mkononi wakati Stand United wao wamekusanya pointi 20 huku Yanga ikiwa na pointi 15 na mechi mbili za viporo mkononi.

Post a Comment

 
Top