BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda
LIGI Kuu ya Vodacom inaendelea leo baada ya mitanange kadhaa kutopigwa mwishoni wa juma lililopita ili kupisha mechi za kimataifa. Viwanja ambavyo vinatarajiwa kuvuta hisia za watu wengi ni Uhuru Dar es Salaam, Sokoine Mbeya na Kambarage Shinyanga.

Yanga wataanza rasmi kuutumia uwanja wa Uhuru kwa kuwakaribisha wakata miwa wa Manungu, Mtibwa Sugar huku watani zao wa jadi Simba wamesafiri hadi jijini Mbeya kuwakabili 'Wagonga Nyundo' Mbeya City. Azam ambayo haijapata matokeo mazuri hivi karibuni yenyewe ipo Shinyanga kuwakabili Stand United wanaoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi inayoongozwa na Simba.

BOIPLUS inakuletea orodha ya wachezaji ambao leo wakiachwa 'wanywe juisi' uwanjani basi wanaweza kuleta kilio kwa timu pinzani hasa katika kipindi hiki ambacho ligi imekuwa ngumu na kwamba ukiteleza kidogo basi unatupwa mbali kwenye msimamo wa ligi. 

YANGA vs MTIBWA SUGAR
Yanga inashika nafasi ya sita kwenye msimamo baada ya kucheza michezo sita pekee, leo ipo nyumbani ikiwa na hasira za kushindwa kuifunga Simba 'pungufu' juma lililopita. Leo mastaa wa mabingwa hao watetezi wataingia uwanjani wakiwa na lengo moja tu, kuwafurahisha mashabiki wao.
Walinzi wa Mtibwa hawapaswi kufumba macho mbele ya hawa wafuatao;

AMISSI TAMBWE
Ukipita katika vijiwe vya soka, wawe mashabiki wa Yanga au hata wa Simba, utasikia "Jamaa analijua goli yule". Hii si sifa ya bure, ni kweli Tambwe si mtu mzuri akikaribia eneo la hatari la timu pinzani. 

Katika mchezo uliopita dhidi ya Simba, alifunga bao la Yanga ambalo licha ya kulalamikiwa kuwa aliumiliki mpira huo kwa mkono, lakini ukitazama video ya tukio hilo utagundua kuwa hata asingeunawa, bado alikuwa ameshafanikiwa kuwatoka walinzi wa Simba kwavile mpira uliwapita kwanza ndipo akaunawa. Huyu asipochungwa ana 90% ya kuwaliza Mtibwa.

OBREY CHIRWA
Kuna uwezekano mkubwa wa straika huyu kugeuka nyota wa mchezo wa leo. Chirwa anabakia kuwa mchezaji hatari  katika kikosi cha Yanga licha kuwa hadi leo hajafanikiwa kuifungia bao lolote timu hiyo huku akiwekwa benchi katika michezo kadhaa.

Anachohitaji Chirwa ni kukaa sawa kisaikolojia na kupotezea matarajio makubwa waliyokuwanayo mashabiki wa Yanga kwake. Kitendo cha kukaa benchi mechi kadhaa kinaweza kuwa kimemfanya atulize akili hivyo leo akaingia kama mpya. Mtibwa wakichezanae kama 'Galasa' watashangaa yeye ndiye anageuka kuwa nyota wa mchezo huo.

Watu wengine ambao hawapaswi kusahauliwa ni kiungo Thaban Kamusoko mwenye uwezo mkubwa wa kupandisha timu pamoja na mawinga Simon Msuva na Juma Mahadhi.

Mtibwa yenyewe imetulia nafasi ya tatu baada ya kukusanya pointi 14. Yanga hawapaswi kuwadharau wakata miwa hao kwavile misimu yote wamekuwa wakifanya vizuri sana mzunguko wa kwanza ingawa 'hukata moto' mzunguko wa pili.
RASHID MANDAWA
Ameshapachika mabao matatu nyavuni hadi sasa, si mchezaji wa kubeza hata kidogo. Kama ilivyo kwa Ngoma wa Yanga, Mandawa pia ana nguvu lakini pia ana maamuzi ya haraka.

Walinzi wa Yanga hawapaswi kuhisi wanacheza na mshambuliaji wa kawaida, watatoka vichwa chini kwavile straika huyu ana uwezo mkubwa wa kubadili matokeo dakika yoyote.

HARUNA CHANONGO
Ni kama vile amerudi tena kwenye 'game' baada ya kutokuwa kwenye kiwango bora kwa kipindi kirefu. Winga huyu wa zamani wa Simba na Stand United amekuwa katika kiwango bora tangu ajiunge na Mtibwa huku licha ya kufunga mabao mawili, amekuwa chachu katika upatikanaji wa mabao mengine.

Chanongo anaonekana kuivaa sawia mikoba iliyoachwa na Shiza Kichuya aliyetimkia Simba, walinzi wa pembeni wa Yanga wanapaswa kuwa makini wanapojaribu kupanda kushambulia, wakimsahau Chanongo yanaweza kuwa mengine.


MBEYA CITY vs SIMBA SC
Huu ni mtanange mwingine wa kukata na shoka leo, huko jijini Mbeya wanasema "Mtoto hatumwi dukani labda kununua pipi yake tu". Jiji limepambwa kwa rangi mbili tu, nyekundu na zambarau huku shamrashamra zikiwa zimeanza mapema.

Miaka yote mechi hii imekuwa na mvuto sana lakini mwaka huu 'mzuka' umeongezeka hasa kwavile Simba hawajaenda Mbeya kama wanyonge tena, wanaongoza ligi tena wakiwa hawajapoteza mchezo wowote huku uhakika wao wa kupata ushindi ukichagizwa na kiwango bora cha nyota wake kadhaa.SHIZA KICHUYA
Hii haipingiki, Simba wameanza kuiona jezi namba 25 yenye ubora waliyoi'miss' kwa miaka kadhaa tangu ivuliwe na Emmanuel Okwi. Sasa wanaiona tena ikiwa imevaliwa na mtu anayeelekea kufanana tabia na Okwi, tabia ya kuamua matokeo hata pale zinapoonekana dalili za kukata tamaa.

Kichuya aliipa Simba pointi tatu kwa bao lake pekee dhidi ya Azam FC, lakini kama haitoshi akaihakikishia pointi moja muhimu dhidi ya Yanga kwa bao la 'kideoni' la dakika za lala salama.

Kwa hali hii walinzi wa City wanatakiwa waingie uwanjani wakijua kuna Okwi mpya ndani ya Simba. Si ajabu Kichuya akaamua matokeo ya mchezo wa leo aidha kwa kufunga bao au kusababisha kama tu City watamchukulia 'poa' kijana huyo mwenye umbo dogo lakini aliyebarikiwa kasi na akili nyingi.

LAUDIT MAVUGO
Najua utashangaa kuona jina la straika huyu kutoka Burundi kwenye orodha ya wachezaji wa kuchungwa sana leo, na hii ni kwasababu hajawa kwenye kiwango bora hivi karibuni. Lakini kiuhalisia huyu yupo kwenye nafasi kubwa sana ya kuipatia ushindi Simba kama walinzi wa City hawatokuwa makini.

Mavugo ndiye mchezaji wa Simba anayeongoza kwa kuwa na maamuzi ya haraka, tatizo lake ni kujaribu kufunga hata mahali ambapo si rahisi. Lakini mara zote mabao yake yametokana na maamuzi yake ya haraka. Ila pale maamuzi yake yanapogonga ukuta ndipo minong'ono inapoanza.

Leo anaingia katika uwanja ambao licha ya kwamba utajaa lakini idadi ya watazamaji haitofikia wale wanaoingia uwanja wa Taifa, kwa mantiki hiyo hatokuwa kwenye presha kubwa ya mchezo, hali itakayomfanya atulie na kufanya kile kinachotarajiwa na wekundu hao wa Msimbazi.

Kwa upande wa Mbeya City wao licha ya kwamba wapo nyumbani, bado wanajivunia kuanza vizuri ligi ingawa wamelazimishwa sare ya bila mabao dhidi ya Stand United juma lililopita. Sare hiyo katika uwanja wa nyumbani haipaswi kuwapa matumaini Simba kwavile wagonga nyundo hao wana nyota hatari wanaoweza kuwarejesha Dar kimya kimya.DITRAM NCHIMBI
Hatajwi sana lakini ni kijana hatari ambaye licha ya kasi na uwezo wa kumiliki mpira, bado ni mzuri anapolikaribia lango. Simba wakimsahau huyu watalia kweli kwavile sifa yake kubwa ni kutotabirika anachotaka kufanya.

JOSEPH MAHUNDI
Huyu ni nyota mwingine ambaye amezoeana vema na wachezaji wenzake katika kikosi cha City, anajua wanahitaji nini na wao wanajua anachohitaji. 

Kwa kikosi cha Simba ambacho kina wachezaji wapya wengi ni lazima wawe makini sana na watu waliocheza pamoja muda mrefu. Hapa unahitajika ulinzi wa kiwango cha juu hasa pembeni mwa uwanja ambako nyota huyu hupenda kushambulia akitokea huko.

Post a Comment

 
Top