BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
NI kama umebaki mwezi mmoja pekee mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom umalizike huku timu mbalimbali zikiingia kwenye usajili wa dirisha dogo ambao kikawaida inakuwa ni kufanya marekebisho madogo tu ya vikosi vyao hasa pale walipoona kuna mapungufu.

Lakini imebainika kwamba timu kongwe za Simba na Yanga ndizo zinazoonekana  kuwa na kazi ya ziada kuwabana nyota wao ili wasisajiliwe na timu pinzani kwani wengine wao ifikapo kipindi hicho watakuwa wamebakiza miezi sita tu ya kuzitumikia na kikanuni wanaruhusiwa kufanya  mazungumzo ya usajili mpya na timu yoyote bila timu wanazochezea kuambulia chochote.

Nyota wa Simba ambao mikataba yao inakwenda ukingoni ni Ibrahim Ajib, Said Ndemla, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Janvier Bokungu na Manyika Peter Jr, hapa ni wawili tu ambao hawapo kwenye kikosi cha kwanza, Ndemla na Manyika.

Kwa upande wa nyota hao wa Simba tayari baadhi yao wamefanya mazungumzo na uongozi kwa ajili ya kuongeza mikataba akiwemo Zimbwe Jr na Ajib ambao wana uwezekano mkubwa dirisha dogo wakapewa mikataba mipya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe na viongozi wenzake wameonyesha kutokuwa na hofu juu ya wachezaji ambao mikataba inakwenda ukingoni na kwamba hivi sasa wamewekeza nguvu zao kwenye mechi za ligi kuu.Rais wa Simba, Evans Aveva pia aliwahi kutamka kuwa mazungumzo na baadhi ya nyota wao akiwemo Zimbwe Jr yamekamilika bado kusaini tu hivyo hawana hofu na hawa wengine wanasubiri taarifa ya kocha Joseph Omog kama itakuwa na mapendekezo ya kufanya marekebisho kama kuongeza ama kupunguza ingawa changamoto kubwa kwa Simba ni beki wa kulia.

Nafasi hiyo ilikuwa ikitumikiwa na Hamad Juma ambaye bado hajakaa vizuri kiafya baada ya kuanguka bafuni na kuchanika kichwani na sasa inachezwa na Bokungu ambaye amesaini mkataba wa miezi sita unaomalizika Desemba hivyo ana changamoto ya kulishawishi benchi la ufundi ili aongezewe mkataba, vinginevyo anaweza kupoteza nafasi.

Yanga yenyewe inaweza ikawapoteza nyota wao Donald Ngoma, Vincent Bossou, Thaban Kamusoko, Deus Kaseke, Matheo Anthony na Mwinyi Haji wote wapo kikosi cha kwanza isipokuwa Matheo aliyesajiliwa akitokea KMKM ya Zanzibar. Ngoma aliwahi kupata dili msimu uliopita katika moja ya timu zinazoshiriki ligi kuu nchini Yugoslavia lakini ilielezwa kuwa bosi wa Yanga alitaka auzwe kwa dola 350,000 zaidi ya Sh 700 milioni.Ukiachana na Simba pamoja na Yanga, Azam FC ina beki wao Paschal Wawa ambaye msimu uliopita aliisaidia sana timu hiyo tofauti na msimu huu ambapo hajacheza mechi hata moja na mkataba wake unamalizika Desemba, Wawa atakuwa huru kusaini mkataba na timu yoyote na tayari Yanga ni miongoni mwa timu ambazo zinatajwa kuwania saini yake ukiachana na timu za nje ambazo pia zinahitaji huduma yake.

Beki huyo pia alidaiwa kutaka kurudi kwenye timu yake ya zamani ya Al-Merrikh lakini mpango huo ulikuwa ukikwama kutokana na mkataba wake na Azam ingawa hadi sasa inasemekana ana nafasi ya kurejea huko kama mipango yake mingine itakwama.Yanga na Azam zimekuwa na mwenendo usioridhisha kwenye ligi huku upande wa Yanga ikidaiwa kuwa wachezaji wao wamekuwa na uchovu wa mwili kwani hawajapumzika tofauti na timu nyingine wakati Azam yenyewe ikidaiwa mfumo wa makocha wapya ndiyo unaoigharimu.

Kutokana na mwenendo huo, viongozi wa timu hizo zote wameonekana kupambana zaidi kwenye ligi bila kujali mikataba ya wachezaji wao ambao wengine ni tegemeo kwenye vikosi vyao, Simba ina kiu ya kutwaa ubingwa ndiyo maana hawana presha hasa pale wanapoangalia kikosi chao kuwa imara msimu huu.

Post a Comment

 
Top