BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Dar
USHINDI raha sana! Simba wana pointi 29 kibindoni na wana mechi mbili za Kanda ya Ziwa, watacheza na Mwadui pamoja na Stand United ila uongozi wa timu hiyo umeona usiwachoshe wachezaji wao na kuamua kuwapandisha 'pipa' hapo kesho saa 9 alasiri kwenda Mwanza na baadaye kuunganisha Shinyanga.

Ikumbukwe kwamba Simba wamecheza mechi 11 bila kupoteza jambo ambalo linawapa matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa unaoshikiliwa na Yanga ambayo msimu huu mwenendo wake si mzuri japokuwa inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 21 sawa na Stand ila ni tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Habari nzuri kwa wachezaji wa kikosi cha Simba kesho ni kupanda Ndege ambayo hawajafanya hivyo kwa zaidi ya miaka mitatu ambayo walikuwa wamepoteza ubora wao kwenye ligi, hawakupanda kwenda mechi za ligi kuu Bara zenye umbali mrefu kama Mbeya na Kanda ya Ziwa ama mashindano ya kimataifa tofauti na watani zao Yanga ama Azam ambao kwao ni kawaida. Hii sasa Simba wameanza kukata ngebe za wapinzani wao.

Oktoba 29,Simba watacheza na Mwadui  huku mechi yao ya pili dhidi ya Stand United itachezwa Novemba 2 kwenye uwanja wa CCM Kambarage.

Ni safari ndefu ingawa wachezaji wa Simba ukiachana na wale wa kigeni ambao kupanda Ndege ni jambo la kawaida wanapokwenda likizo ama kwenye timu zao za Taifa na wale ambao wamewahi kubahatika kuitwa Taifa Stars basi kesho watatumia saa 1:45 tu kufika Mwanza na kuunganisha Shinyanga wanakokwenda kusaka pointi sita.

Viongozi wa Simba, Makamu wa Rais, Gofrey Nyange Kaburu na Haji Manara (msemaji wa Simba) wote walithibitisha timu yao kuondoka kesho kusaka pointi hizo sita.Kikosi cha watu 21 ndicho kitakachoondoka ambao ni Vincent Angban, Manyika Peter Jr, Janvier Bokungu, Mohamed Hussein, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya, Jamal Mnyate, Ibrahim Ajib, Laudit Mavugo, Said Ndemla, Ame Ally, Hamad Juma, Abdi Banda, Emmanuel Semwanza na Mzamiru Yassin pamoja na benchi la ufundi.

Post a Comment

 
Top