BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
UONGOZI wa klabu ya Simba umefanya kikao cha faragha na Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye kuzungumza mambo mbali mbali huku wakikataa kuweka wazi.

Msafara huo uliongozwa na Rais Evans Aveva Makamu wake Gofrey Nyange 'Kaburu' Katibu Mkuu Patrick Kahemele pamoja na msemaji wa klabu hiyo Haji Manara.

BOIPLUS imewatafuta viongozi hao ili kujua dhumuni la kikao hicho cha faragha lakini simu zao za mkononi ziliita bila kupokelewa labda kutokana na 'unyeti' wa kikao hicho.

Habari za ndani zinasema kuwa Uongozi  huo umeenda kuomba kuendelea kutumia Uwanja wa Taifa baada ya kufungiwa kutumia kufuatia mashabiki wake kung'oa viti vya dimba hilo la kisasa.

Oktoba mosi kwenye mchezo dhidi ya watani wao Yanga mashabiki hao waling'oa viti 1781 baada ya kutoridhishwa na maamuzi ya refarii Martin Saanya ya kukubali goli la mshambuliaji Amissi Tambwe ambalo aliushika mpira kabla ya kufunga na kumuonyesha kadi nyekundu nahodha Jonas Mkude.

Wiki iliyopita Msemaji wa klabu hiyo alisema kwenye mkutano wa waandishi wa Habari kuwa wamemuandikia barua Waziri kumuomba msamaha kwa tukio lile huku wakimtaka aende hadi kwa Rais wa nchi kuwaombea radhi kutokana na tukio hilo lililofanywa na mashabiki wake.

Baada ya vurugu Oktoba 2 Waziri Nape alisitisha matumizi ya uwanja huo kwa timu za Simba na Yanga huku akizuia mapato ya mchezo huo hadi watakapo lipa Huduma za marekebisho ya uwanja huo.

Post a Comment

 
Top