BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Dar
CHAMA cha Waamuzi Tanzania (FRAT) kimelitaka Shirikisho la Soka nchini (TFF) kumwondoa kwenye ratiba ya kuchezesha mechi zote za Ligi Kuu ya Vodacoma ambazo amepangwa mwamuzi Martin Saanya kwa madai kuwa aliharibu mechi ya Simba na Yanga kutokana na kutokuwa kwenye kiwango cha kumudu mechi hiyo. 

Saanya alichezesha mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 huku akizua mtafaruku mkubwa kwa wachezaji baada ya Amissi Tambwe kufunga bao la utata linalodaiwa kuwa si halali kwani aliunawa mpira kabla ya kufunga.

Baada ya kukubali bao hilo wachezaji wa Simba walimzonga mwamuzi huyo kupinga uamuzi wake ndipo hapo Saanya aligawa kadi nyekundu kwa nahodha Jonas Mkude ikidaiwa kuwa alimsukuma mwamuzi huyo.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FRAT, Kanali Isaro Chacha alisema kuwa wanashangazwa na kitendo cha TFF na Bodi ya Ligi kumpa mechi kubwa Saanya wakati ametoka kifungoni na hajachezesha mechi hata moja hivyo wanapaswa kubeba lawama na mwamuzi huyo kupewa adhabu ya kuondolewa kwenye ratiba.

"Mwamuzi mwenye beji ya FIFA hawezi kuchezesha mechi kwa makosa kiasi kile, Saanya hapaswi kuchezesha mechi za ligi, TFF wamuondoe kwenye ratiba ya msimu mzima, makosa waliyofanya TFF ni makubwa kwani Saanya ametoka kwenye dhabu ya kifungo hajachezesha mechi hata moja unampaje mechi kubwa kama hiyo.

"Tunadhani Saanya pengine alichezesha kwa maelekezo ya TFF kwani Yanga hawajampa pesa ili awabebe. Amekataa bao la wazi la Ibrahim Ajibu kakubali bao la Tambwe ambapo alitakiwa ampe kadi ya njano kwa kushika mpira kwa mkono, mbaya zaidi akatoa kadi nyekundu kwa nahodha wa Simba, hayo ni mapungufu makubwa kwa Saanya. 

"Kama Mkude alifanya kosa angempa kadi ya njano kwani yule ni nahodha, tunakwenda wapi na mpira huu, watoe adhabu kwa kuangalia marudio ya mechi, taarifa ya msimamizi wa mechi pamoja na ya mwamuzi," alisema Kanali Chacha.

Chacha alisema kuwa chama chao kinakosa nguvu kwasababu mamlaka yote yamekumbatiwa na TFF na ndio wamechukuwa jukumu la kuwapangia waamuzi mechi na si wao kama ilivyokuwa hapo awali.

Alisema kuwa Simba wana kila haki ya kulalamika juu ya vitendo walivyofanyiwa kwani haki yao ya wazi walinyimwa.

Post a Comment

 
Top