BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
WIKI mbili baada ya kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' kujiuzulu kufundisha timu ya Mwadui FC wachezaji wa timu wameshaanza kumkumbuka kocha huyo mtaalamu wa kucheza na akili za wapinzani kwa kutumia maneno.

Julio alijiuzulu kufundisha mpira  kutokana na kile alichodai kuwa ni waamuzi kushindwa kuchezesha kwa haki huku wakiziingizia timu hasara baada ya kufanya maandalizi makubwa na kusafiri umbali mrefu kutafuta alama tatu huku matokeo yakiwa tayari yamepangwa.

Kiungo wa timu hiyo Abdallah Seseme ameiambia BOIPLUS kuwa hakuna mchezaji yoyote aliyefurahishwa na kitendo cha kocha huyo kujiuzulu kwavile alikuwa na mchango mkubwa kuanzia kuhamasisha na hata ushauri kwa wachezaji kitu ambacho wanakikosa kwa sasa.

"Hatuwezi kuingilia maamuzi yake ila kiukweli 'tunammisi', bado tutaendelea kupigana ili kuhakikisha Mwadui inaendelea kufanya vizuri hata bila ya uwepo wake," alisema Seseme.

Mwadui tayari wapo jijini Dar es Salaam tangu jana usiku wakiwavutia kasi Maafande wa JKT Ruvu katika mchezo utakaopigwa kesho kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani ambapo wenyeji wamejipanga kuwachezesha kwata baada ya kufanya marekebisho kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Tangu Julio ajiuzulu 'Wachimba madini' hao wamecheza mechi moja ambayo ni dhidi ya African Lyon na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Mwadui Complex.

Post a Comment

 
Top