BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu, Chamazi
BENCHI la ufundi la Azam FC limeshusha pumzi baada ya kushudia timu yao ikiibuka na ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya Maafande wa JKT Ruvu kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex.

Azam walicheza michezo sita mfululizo bila kupata ushindi zaidi ya kuambulia vipigo na sare hata kwenye dimba hilo hali iliyoanza kuzusha minong'ono kutoka kwa mashabiki wa 'Wana lambalamba' hao na kuhoji kuhusu uwezo wa Kocha Zeben Hernandez raia wa Hispania pamoja na benchi lake.

Azam walikuwa na matarajio makubwa kutoka kwa Mhispania huyo kutokana na historia ya nchi yake kucheza soka safi la kueleweka lakini tangu Mkufunzi huyo kutua kwa Mabingwa hao wa ligi mara moja hali imekuwa tofauti baada ya kushinda michezo minne pekee katika mechi 11iliyoshuka dimbani huku wakicheza soka la kawaida.

Nahodha John Bocco 'Adebayor' ndiye aliyeipatia Azam bao hilo kwa mkwaju wa penalti dakika ya 57 baada ya mchezaji mmoja wa Maafande hao kuunawa mpira katika harakati za kuokoa hatari langoni mwao.

Ruvu walikuwa na nafasi ya kuweza kurudisha bao hilo lakini safu ya ushambuliaji ilikuwa butu ambapo mara kadhaa Kocha wa Maafande hao Malale Hamsini amekuwa akiipigia kelele kutokana na kutengeneza nafasi nyingi lakini wanashindwa kuzitumia hali inayopelekea kupata matokeo yasiyoridhisha.

Kiungo Hassan Dilunga alipata nafasi ya kuifungia timu yake goli lakini shuti lake lilipanguliwa vyema na mlinda mlango Aishi Manula na kuwa kona tasa.

Katika mchezo huo kiungo Himid Mao alioneshwa kadi nyekundu na mwamuzi dakika ya 85 baada ya kumchezea rafu mbaya Rahim Jumaa.

Post a Comment

 
Top