BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
MCHEZAJI yoyote akicheza Simba na Yanga huamini safari yake ya kwenda Ulaya imefika. Hiyo ni kwasababu timu hizo ni kubwa na ni rahisi wachezaji wao kuuzwa tofauti na wanapokuwa kwenye timu nyingine ndogo ingawa katika miaka ya hivi karibuni Azam imeongeza upinzani.

Hata hivyo, Simba na Yanga ndizo timu pekee ambazo zinaongoza kwa kutema wachezaji kwasababu mbalimbali na wachezaji hao wanapokwenda timu nyingine huwa wanafanya vizuri na kutoa mchango mkubwa kwa timu husika.

Hawa hapa ni baadhi ya nyota waliowahi kucheza Simba na Yanga na wanafanya vyema kwenye timu zao za sasa.

Shaban Kisiga 'Marlon' - Ruvu Shooting
Huyu ni kiungo ambaye Simba na Mtibwa Sugar ilikuwa kama nyumbani kwake, kwamba akikosa huku basi maisha yake yataendelea sehemu nyingine bila wasiwasi, hiyo ni kutokana na kiwango chake na popote pale anapokwenda kazi yake inakuwa ni moja tu, kuing'arisha safu ya kiungo.

Kisiga ambaye ni mtaalamu wa kupiga mashuti ya mbali yanayozaa matunda amewahi pia kuchezea timu za Azam FC, SC Villa pamoja na timu  moja ya nchini Oman ambapo alipotoka huko aligombewa na timu za Simba na Mtibwa.

Kujitunza kwa Kisiga mpaka sasa kulimfanya aisaidie Ruvu Shooting kupanda daraja baada ya kuondoka Simba katika mazingira ya kutatanisha.

Kiungo huyo aliondoka Simba kutokana na misimamo aliyonayo ya kisoka na maisha yake huku akikiri kwamba hapendi kuona haki yake inapotea ama anafanyiwa uonevu pasipokuwa na sababu za msingi, anajiamini kiwango chake na ni mkongwe ambaye mpaka sasa anafanya vizuri kwa dakika zote 90 anazopewa, Kisiga ni miongoni mwa nyota tegemeo ndani ya Ruvu Shooting mpaka sasa.

Geofrey Taifa - Kagera Sugar
Naye ni mkongwe katika soka la Bongo, alianzia soka lake katika timu ya Ashanti United 'Watoto wa Ilala' na mwaka 2008 alijiunga na Kagera Sugar aliyoitumikia hadi mwaka 2011 ndipo Yanga walipoona kuna haja ya kumsajili kwani tayari alikuwa katika kiwango kizuri zaidi.

Taita aliitumikia Yanga kwa mafanikio makubwa hadi walipoachana naye na kuamua kwenda kuipandisha daraja Majimaji ingawa msimu huu Taita amerudi kuichezea timu yake ya zamani ya Kagera Sugar hiyo ni kutokana na sababu kwamba Taita bado anajitambua na anatunza kipaji chake ndiyo maana anapewa nafasi hadi sasa.

Nasoro Masoud 'Chollo' - Mwadui FC
Beki wa kulia wa Mwadui FC, Nassoro Masoud 'Chollo' naye huwa hakubali kuchuja kirahisi rahisi tu. Amecheza miaka nane hadi sasa tangu aanze soka lake la kiushindani mwaka 2008 akiwa na Moro United, huenda pia amepita timu nyingi lakini ndani ya Simba ambayo ilimsajili mwaka 2011 alicheza kwa nidhamu kubwa.

Chollo amepitia mikononi mwa makocha wengi akiwa Simba, akiwemo Zdravicko Logarusic, Patrick Phiri, Julio, Abdallah Kibadeni na aliwahi kuwa nahodha wa muda mrefu tu ndani ya Simba kabla ya kumaliza mkataba wake. Chollo alikwenda kujiunga na Stand United msimu uliopita chini ya kocha wake wa zamani akiwa Simba, Patrick Liewig kwa mkataba wa mwaka mmoja tu na alicheza mechi chini. Msimu huu Chollo yupo Mwadui FC na ni nahodha wa timu hiyo.

Henry Joseph - Mtibwa Sugar
Ni kiungo mkongwe pia, alisajiliwa Simba mwaka 2006 ambapo aliichezea hadi 2009 na badaye kuuzwa katika klabu ya Kongsvinger aliyoichezea hadi mwaka 2013 alipoamua kurejea nyumbani baada ya mkataba wake kumalizika, Henry kituo chake cha kwanza alipotua nchini ni kujiunga na timu yake ya zamani ya Simba.

Hata hivyo, Henry hakuweza kuitumikia sana timu hiyo baada ya kumpa makataba wa mwaka mmoja pekee na alipomaliza mkataba huo Simba waliamua kuachana naye na ndipo alipojiunga na Mtibwa Sugar msimu wa 2014 ambapo anaichezea hadi sasa.

Makocha wa Mtibwa Sugar akiwemo Mecky Mexime alipokuwa na kikosi hicho alikuwa anapewa kumwanzisha Henry lakini baadaye alifanya mabadiliko na kumwingiza mkongwe mwenzake Shaban Nditi ama anaanza Nditi halafu Henry ataingizwa baadaye. Ingawa kasi yake si kama alivyokuwa Simba ila bado makocha wa Mtibwa Sugar wanamwamini.

Salum Kanoni - Mwadui FC
Kanoni alijiunga Simba msimu wa 2009 ambapo alicheza hadi 2011 walipoamua kumpeleka kwa mkopo Kagera Sugar. Hiyo ni baada ya kuona kiwango chake kwa wakati huo kimeshuka. Ila mkataba wake ulipomalizika Simba hawakuonyesha nia ya kumrejesha beki huyo kikosini kwao.

Kagera Sugar wao waliona wameokota dhahabu, walimpa mkataba baada ya huo wa mkopo kumalizika, Kanoni amefundishwa na makocha tofauti hasa Jackson Mayanja ambaye sasa yupo Simba pamoja na Mrage Kabange aliyekuwa msaidizi wa Mayanja. Kanoni bado yupo kwenye ubora wake ametua Mwadui FC baada ya kukaa kwa kipindi kirefu na Kagera Sugar, yupo kwenye kikosi cha kwanza cha Mwadui.

Amri Kiemba - Stand United
Kiemba amepita timu nyingi zikiwemo Yanga, Simba na Azam ukiacha na timu yake ya kwanza ya Moro United. Kiemba amepitia mapito mengi katika soka hasa akiwa Simba lakini amekuwa ni mchezaji asiyekata tamaa anapambana bila kushusha kiwango chake.

Kwasasa anaichezea Stand United ambayo aliingia nayo mkataba wa miaka miwili na sasa ndiyo anamalizia mkataba wake huo, Kiemba ni miongini mwa wachezaji ambao Kocha Patrick Liewig amekuwa akiwakubali kutokana na nidhamu yake, yupo kwenye kikosi cha kwanza tangu asajiliwe Stand na ikitokea hajacheza basi ana sababu za msingi majeruhi.

Ramadhan Chombo 'Redondo' - Mbeya City
Mbeya City imemsajili Redondo tangu msimu uliopita na sasa wamemuongeza mkataba wa mwaka mmoja msimu huu. Redondo umri wake umeenda ila kocha Kinnah Phiri anaamini kuwa ukongwe na uzoefu wake katika ligi ndivyo vinavyombeba kiungo huyo.

Redondo ambaye aliwahi kuichezea Simba na Azam kwa nyakati tofauti amekuwa na msaada ndani ya Mbeya City hasa pale ambapo Phiri anaona maji yamemfika shingoni hivyo humwingiza Redondo kuokoa jahazi ingawa hampi dakika nyingi ila ni tegemeo kubwa kwake.

Danny Mrwanda - Kagera Sugar
Kwa miaka ya nyuma, Mrwanda ndiye alikuwa mchezaji ghali kuliko wote katika soka kutokana na kulipwa vizuri alipokwenda kucheza soka la kulipwa nchini Vietnam, pia amewekeza sana ingawa sasa hivi amepigwa bao na Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji. Ila bado pia Mrwanda aliweka heshima kutokana na kucheza soka kwa nidhamu ya juu.

Utamu wa Mrwanda hadi sasa bado haujaisha, bado ana uwezo wa kucheza kwa dakika nyingi kutokana na kukosekana kwa wachezaji wenye uwezo wa kutunza vipaji vyao kwa miaka ya hivi karibuni kama ilivyokuwa kwa mkongwe huyo.

Mrwanda aliichezea Al Tadamon, Ðong Tâm Long, Hoàng Anh Gia Lai zote za Vietnam, Simba, AFC Arusha, aliipandisha Majimaji na sasa yupo Kagera Sugar ambako anacheza kwa kiwango kizuri ingawa jua limeanza kuzama.  

Haroun Chanongo - Mtibwa Sugar
Kiungo huyo aliwahi kwenda kufanya majaribio TP Mazembe ya DR Congo mwanzoni mwa mwaka huu, aliporudi huko alikutana na utata wa Liewig wakati huo yupo Stand United, mara nyingi Liewig alikuwa akimuweka benchi Chanongo kwa madai kuwa na utovu wa nidhamu.

Stand United ilimsajili Chanongo akitokea Simba, kwanza alipelekwa kwa mkopo na baadaye wakampa mkataba lakini maisha yake ndani ya Stand yalikuwa magumu na kupelekea kushusha kiwango chake. Hivi sasa kiungo huyo yupo Mtibwa Sugar na anaonekana kurejesha kiwango chake cha mwanzo. Chanongo amefunga mabao matatu.

Edward Christopher - Kagera Sugar
Msimu uliopita aliifungia Toto Africans ya jijini Mwanza mabao matano. Alipomaliza mkataba wake aliamua kwenda Kagera Sugar ingawa bado hajafanikiwa kutikisa nyavu. Edo ni zao la Simba ambalo lilifanya vizuri kabla ya kuachana naye kwa madai ya kushuka kiwango. Straika huyo anafanya vizuri kwenye timu hiyo ambapo ameonekana kupambana kurejesha kiwango chake cha awali. Aliwahi pia kuichezea Polisi Moro.

Wengine ambao wamekuwa waking'ara na timu nyingine wakiwa wametokea Simba na Yanga ni Abdallah Seseme (Mwadui), Said Bahanuzi na Hussein Javu (Mtibwa Sugar).

Post a Comment

 
Top