BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Yanga imeutangaza Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuwa uwanja wake wa nyumbani kwa mechi za ligi kuu Tanzania bara na michuano mingine baada ya kufungiwa Serikali kutumia dimba la Taifa.

Simba na Yanga zimefungiwa kutumia uwanja wa Taifa baada ya mashabiki wao kufanya fujo na kuvunja mageti manne pamoja na viti 1781 katika mchezo dhidi ya watani hao uliofanyika Octoba mosi.

Mapema wiki iyopita Yanga ilipeleka maombi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kutumia Uwanja wa Amani kwa michezo yake ya ligi lakini kutokana na kanuni kutoruhusu ndiyo wakaamua kutumia Uwanja huo. Jumatano Oktoba 12 mabingwa hao watashuka dimbani hapo kumenyana na Mtibwa Sugar katika muendelezo wa ligi kuu ya Vodacom.

Michezo mingine itakayopigwa Jumatano ni kati ya Mbeya City dhidi Simba mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika mchezo unasubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na Wekundu hao kuwa kwenye kiwango bora lakini tangu City ipande daraja msimu mwaka 2014/15 wamekuwa wakiwapa shida hasa katika dimba hilo.

Tayari City kupitia kwa mabeki wake Hassan Mwasapili na Haruna Shamte wamesema safu ya ushambuliaji ya Simba inayoongozwa na Ibrahim Ajib pamoja na Laudit Mavugo isitegemee mteremko kwakua wamejipanga kuwathibiti ili wasiwe na madhara langoni mwao. Simba ndiyo kinara wa ligi hiyo ikiwa na alama 17 tayari wamewasili jijini humo kwa ajili ya mchezo huo.

Mtanange mwingine utakuwa mkoani Ruvuma ambapo Majimaji itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.

Mkoani Shinyanga Stand United itaikaribisha Azam FC kwenye Uwanja wa CCM Kambarage huku Mwadui ikiwa mwenyeji wa African Lyon kwenye dimba la Mwadui Complex. Mwadui watashuka dimbani bila ya Kocha wao Mkuu Jamhuri Kihwelo Julio' aliyetangaza kujiuzulu wiki iliyopita kufundisha soka kutokana na waamuzi kuchezesha bila kufuata sheria 17 za soka na kuonekana kupendelea upande mmoja.

Jijini Mwanza Jumatano kutakuwa na ‘Mwanza Derby’ kati ya Mbao FC dhidi ya Toto Africans mchezo utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba  ambapo pilikapilika za jiji hilo zitasimama kwa muda kupisha mtanange huo kutokana timu zote kuamini wanaweza kuondoka na alama zote hali inayoongeza chachu ya mechi hiyo.

Alhamisi Oktoba 13, 2016 Ruvu Shooting itacheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mabatini.

Post a Comment

 
Top