BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
YANGA na Azam zilikwenda Shinyanga wakakutana na kipigo cha wapiga debe wa mji huo, Stand United kila mmoja alifungwa bao 1-0 sasa ni zamu ya Simba kwenda huko ila Wekundu hao waliojikita kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 29 wameshtuka na kujipanga kwenda na mbinu mpya za ushindi ili wasipate aibu kama vigogo wenzao.

Simba yenyewe itacheza mechi mbili, itaanza na Mwadui FC inayoshika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 13 itakayopigwa Oktoba 29 na baadaye Novemba 2, watacheza na Stand United wenye pointi 21 na wanashika nafasi ya tatu, mechi hizo zitachezwa uwanja wa CCM Kambarage ambapo Simba inatarajia kuondoka kati ya kesho au keshokutwa.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema kuwa mabadiliko makubwa ya kikosi cha Simba ndiyo yatawafanya kupata pointi sita mjini humo kama ilivyokuwa mzunguko wa pili msimu uliopita walipoifunga Kagera Sugar na Stand United kwenye uwanja huo.

"Ni lazima twende na mipango ya ushindi, kama tunavyoelezea kila mara kuwa tunahitaji kumaliza mzunguko wa kwanza bila kufungwa, kikosi chetu ni bora na hatupaswi kuangalia wenzetu wamepata nini walipokwenda, sisi tunapigania ushindi tu.

"Hii Simba imeimarika sasa ndiyo maana kila mchezaji anayeingia anafanya vizuri, kwenye timu yetu hakuna mchezaji wa kubadilisha matokeo ndiyo maana hata Mohamed Ibrahim ameanza kwenye kikosi cha kwanza, nikiwa na maana kwamba kila anayetokea benchi anafanya vizuri hata anapoanza.

"Tunachokifanya huwa tunaangalia mechi ipoje na wachezaji wapo katika viwango gani, ndiyo maana wanaoanza mara nyingine wanalazimika kuanzia benchi, huo ni mfumo wetu na wanafanya vizuri kwa kila anayeingia, tunachokihitaji huko mkoani ni pointi sita," alisema Mayanja.

Habari zaidi zinasema kuwa Simba wanaweza kuondoka kwa usafiri wa Ndege ingawa mpaka sasa mpango huo haujakamilika na ikishindikana basi watalazimika kutumia usafiri wa barabara.

Post a Comment

 
Top