BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
YANGA leo imepata ushindi wa bao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu ushindi ambao umeelezwa kuwa ni zawadi ya kocha Hans Pluijm ambaye amejiuzulu kuifundisha timu hiyo kutokana na ujio wa kocha mpya George Lwandamina raia wa Zambia huku kocha wa Maafande hao, Malale Hamsini nusura chozi limtoke kwa kipigo hicho.

Pluijm alikuwepo jukwaani akishuhudia mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Uhuru na kukusanya pointi tatu ambazo zimewasogeza hadi kufikisha pointi 24 wakitanguliwa na Simba yenye pointi 29.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo, kocha msaidizi Juma Mwambusi alisema kuwa kuondoka kwa Pluijm ni pengo kwao lakini hawataacha kupambana ili kupata ushindi kwenye mechi zao zijazo ingawa hata yeye anatajwa kuondoka muda wowote kwani benchi zima litafumuliwa. 

"Mechi haikuwa rahisi kutokana na changamoto zinazotukabili na jinsi mambo yanavyoendelea ndani ya klabu yetu, ila nashukuru wachezaji wameweza kupambana kushinda mabao hayo ambayo tunatoa zawadi kwa Pluijm tuliyeshirikiana naye vizuri kwa kipindi kirefu.

"Kuna pengo ila hatuwezi kupingana na mambo yanavyokwenda, tutamkumbuka sana. Kwa upande wa wachezaji leo waliona mchezo mgumu na ndiyo maana tuliamua kufanya mabadiliko ya mfumo ili kupata mabao," alisema Mwambusi.


Kwa upande wa Malale aliiambia BOIPLUS kuwa, "Katika maisha yangu ya soka sijawahi kufungwa mabao mengi kama ya leo kwa mechi hizi za ndani achana na mechi za kimataifa nilipokuwa na Zanzibar Heroes, nimeumizwa mno na matokeo hayo.

"Mabao yote ya Yanga ni kama tumewagaia maana mabeki wetu hawakuwa makini kabisa leo japokuwa mechi zilizopita walikuwa wapambanaji ila leo wameniangusha tofauti na safu ya ushambuliaji ambayo nimechoka hata kuilalamikia kwa kushindwa kufunga hata wanapokuwa katika nafasi nzuri.

"Hii ni changamoto kubwa kwangu nimefungwa mabao mengi, nipo katika nafasi mbaya sana kwenye msimamo sijazoea hali hii ila nitapambana nayo kuona ni jinsi gani tunajinasua ndiyo maana nimejikuta naingiwa na uchungu ambao ungenitoa machozi," alisema Malale.

Post a Comment

 
Top