BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
AFRICAN Lyon wameharibu mpango wa Simba wa kumaliza mzunguko wa kwanza bila kupoteza mchezo baada ya hii leo kuwafunga bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Simba ambao ndiyo vinara wa ligi hiyo walicheza michezo 13 bila kupoteza huku wakishinda mara 11 na kwenda sare miwili na kujikusanyia alama 35 ambazo ni tano mbele ya Yanga wanaokamata nafasi ya pili kutokana na ushindi walioupata wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Tanzania Prisons.

Simba ilitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza lakini ilishindwa kupenya safu ya ulinzi ya Lyon iliyokuwa ikiongozwa na nyota wake wa zamani Hassan Isihaka, Miraji Adam na Omari Salum.

Lyon walifanya mashambulizi mawili ya nguvu langoni kwa Simba ambapo dakika ya 39 Miraji alipiga Mpira wa adhabu pembeni kidogo ya kumi na nane uliogonga mwamba kabla ya Omari Abdallah nae kufanya hivyo dakika ya 45.


Kipindi cha pili Simba walianza kwa kasi kulisakama lango la Lyon lakini bado wakishindwa katika mbinu za kupenya kusalimiana na mlinda mlango Youthe Rostand.

Abdul Msuhi ndiye aliyepeleka kilio kwa Wanamsimbazi baada ya kufunga bao pekee dakika za nyongeza baada ya kumalizia krosi safi ya Rehani Kibingu aliyetokea benchi.

Simba iliwatoa Mohamed Ibrahim, Mwinyi Kazimoto na Laudit Mavugo nafasi zao zikachukuliwa na Ibrahim Ajib, Saidi Ndemla na Jamal Mnyate. Lyon iliwapumzisha Amani Peter,Khalfan Twenye na Abdallah na kuwaingiza Hamadi Manzi,Kibingu pamoja Raizan Hafidh.

Post a Comment

 
Top